Ligue 1 yafutwa rasmi kutokana na kauli ya Waziri Mkuu wa Ufaransa

47

Serikali nchini Ufaransa imeendelea kupiga marufuku mikusanyiko yoyote ile sawa na shughuli za kimichezo mpaka mwezi wa tisa hata kama haitakuwa inahusisha mashabiki bado imepigwa rungu.

Ligue 1 na Ligue 2 hazitaendelea kutokana na tamko hilo la serikali, awali kulikuwa na mpango wa mechi zilizosalia kwenye ligi daraja la kwanza na la pili zichezwe bila mashabiki lakini Waziri Mkuu wa nchini hiyo amesema mechi haziwezi kuchezwa bila uwepo wa mashabiki.

Edouard Philippe ambaye ni Waziri Mkuu amesema msimu wa 2019-20 wa michezo umeisha kwani wanaenda kuweka vikwazo zaidi kuanzia Mei 11 mwaka huu kutokana na janga la virusi vya Corona.

Itakumbukwa kabumbu ilisimamishwa Marchi 13 nchini humo lakini matumaini ya bodi ya uongozi wa Ufaransa ilikuwa ni kurejesha michezo na kuendelea na msimu mwezi Juni 17 ambao ungetamatika Julai 25.

Pamoja na kauli ya Waziri Mkuu bado Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (LFP) halijatoa tamko kuhusu mfumo watakaoutumia kuifuta ligi, kwa maana kuna ule wa kufuta huku bingwa na timu za kushuka zinakuwepo na kuna ule ligi inafutwa bila uwepo wa timu bingwa wala kushuka daraja.

Ligi wakati inasimama Paris St-Germain alikuwa mbele kwa alama 12 dhidi ya timu ya pili ambayo ni Marseille huku raundi 10 zikiwa zimesalia. Mkiani kulikuwa na Toulouse, Amiens, Nimes na St Etienne.

Author: Bruce Amani