Lionel Messi ahusishwa na nia ya kuondoka Barcelona, migogoro ndani ya klabu yatajwa

438

Kwa mujibu wa kituo cha Redio cha Cadena Ser, nahodha na mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi, 33, amesitisha mazungumzo ambayo yalikuwa yanaendelea ya kurefusha mkataba kati yake na klabu hiyo kwa sababu ya kutajwa kuwa chanzo cha migogoro na kutotulia kwa klabu hiyo.

Inaelezwa kuwa Messi kwa hivi sasa amechoka kuonekana kama ndiye chanzo cha kutotulia kwa Barca huku akihusishwa pia kuwapangia majukumu makocha wanaoajiriwa wa timu hiyo.

Pia Messi amekuwa akitajwa kuwa amekuwa akiamuru nani asajiliwe nani asisajaliwe na nani acheze nani asiyecheze jambo linaloonekana kuwa kikwazo kwa baadhi ya viongozi na wachezaji klabuni hapo.

Imetosha, imetosha, amemwambia Mkuu wa kipindi El Larguero kuwa ataondoka Nou Camp mwishoni mwa msimu ujao kutokana na kuchoshwa na kashfa ambazo amekuwa akitupiwa.

Kuna maswali yanakuja akilini ya kama hayo kweli? Messi mbona kama sio wa namna hiyo? Lakini ukitulia na kujiuliza inatokea vipi hii ni ngumu kupata uhalisi wa kile kinachoonekana.

Kuna baadhi ya madai yanasema Messi alikuwa anahitaji kuona uongozi wa Barcelona unamsajili mshambuliaji wa Kifaransa Antoine Griezmann lakini baada ya kumsajili staa huyo hamhitaji tena klabuni hapo. Hili bila shaka litakuwa sio kweli.

Katika maisha ya kawaida imeonekana mara kadhaa Griezmann amekuwa akitoka kwenda kuvinjari sambamba na familia ya Messi na Suarez na kupata chakula cha usiku pamoja hivyo hakuna tofauti yoyote baina ya watu hawa wawili.

Katika tuhuma za kuwa na maamuzi ya makocha pia kuna baadhi ya taarifa zinasema Messi ndiye aliyemfukuzisha kazi Tata Martino na kuwa yupo njiani kumuondoa kocha wa sasa Quique Setien kwa sababu hapendezwi na staili zake za uchezaji sio za kweli pia.

Kama mchezaji anayelipwa zaidi Barcelona kila jambo mbaya linapotokea basi amekuwa akitajwa kuwa anachangia matatizo kama hayo, hasa timu inapopoteza mchezo.

Kiukweli ndani ya klabu kuna matatizo ambayo hayajapatiwa tiba hasa kwa Rais wa timu hiyo Josep Maria Bartomeu, kwa mfano aliahidi kumrudisha Neymar lakini mpaka sasa bado, akasema wanamfukuza kocha Ernesto Valverde ili kumchukua mchezaji wao wa zamani Xavi lakini baadae Rais akatangaza vitu tofauti, ikiwa na kocha mpya ambaye sio Xavi.

Katika mkataba wake wa sasa, Messi ana kipengele kinachomruhusu kuondoka klabuni hapo. Licha ya furaha ambayo familia yake kuishi nchini Hispania lakini binafsi inaonekana hana furaha kama siku za nyuma.

Kabla ya wiki hizi za karibuni na matokeo mabaya ya siku za usoni ya Barcelona kulikuwa na maelewano mazuri na mazungumzo ya mkataba mpya yalikuwa yanaenda vizuri lakini baada ya hapo inaonekana mambo kutokuwa vema kwa Wanacatalunya hao.

Kipi kitafuata:- endapo Messi hatatimiziwa ahadi zake ikiwa ni pamoja na kumrudisha Neymar huenda akaondoka klabuni hapo na kwingineko hasa kipindi kama hiki ambacho PSG na Manchester City zimekuwa zikihusishwa kumhitaji.

Kuja kwa Xavi ndani ya Barcelona huenda kukafufua furaha ndani ya Lionel Messi hivyo kuzalisha amani mpya klabuni, ni kazi ya Josep Maria Bartomeu na viongozi wa juu kuhakikisha staa huyo anasalia klabuni.

Author: Bruce Amani