Lipuli yailipua Yanga na kuitimua katika Kombe la FA

Klabu ya Yanga imeangukia pua baada ya kufungwa goli 2-0 dhidi ya Wanapaluengo Lipuli FC katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la Shirikisho la Azam uliofanyika dimba la CCM Samora Mkoani Iringa leo Jumatatu Mei 6.

Yanga ilikuwa inahitaji ushindi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wowote msimu huu baada ya nafasi ya kushinda taji la ligi kupotea huku Simba akiwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi.

Magoli yote mawili yamefungwa kipindi cha kwanza kupitia kwa Paul Nonga dakika ya 27 akimalizia mpira ulioshindwa kuondoshwa na mabeki wa Yanga ambapo goli la pili pia likifungwa na Daruwesh Saliboko yakihitimisha karamu ya ushindi wa timu hiyo iliyobatizwa jina la salamu maarufu Iringa ya “Kamwene”.

Hii ni mara ya pili Yanga kufungwa na Lipuli katika dimba la CCM Samora baada ya ile ya ligi kufungwa goli 1-0 huku kocha Suleiman Matola akionekana kuziweza mbinu za Yanga.

Kwa matokeo hayo Yanga imetupwa nje ya mashindano ya FA na kuwaachia Lipuli FC kwenda kukutana na Azam FC hatua ya fainali itakayochezwa Mkoani Iringa katika uwanja wa Ilulu.

Hii ni mara ya pili Yanga kuondoshwa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam kwani msimu wa 2017/2018 iliondoshwa na Singida United na sasa na Lipuli.

Matokeo ya kufungwa kwa Yanga yanaingia wakati ambao timu hiyo imefanya uchaguzi ambao kwa kiasi kikubwa umeleta neema kwa timu kwa kuahidiwa milioni 70 endapo ingeibuka na ushindi. Timu hiyo imekaa bila uongozi kwa miaka miwili.

Author: Asifiwe Mbembela