Liverpool, United, Arsenal zapata ushindi muhimu

Vinara wa Premier League Liverpool walitoka nyuma na kushinda mechi ya kusisimua dhidi ya Crystal Palace na kuendeleza mapambano yao ya kunyakua ubingwa wa ligi msimu huu.

Mabao mawili kutoka kwa Mo Salah yaliisaidia Liverpool kuigeuza faida ya kipindi cha kwanza na ijapokuwa vijana hao wa Jurgen Klopp walikuwa wakipambana kuponyoka na ushindi huo wa 4-3 katika dakika za majeruhi, walikamata kabisa usukani na pengo la pointi saba.

Marcus Rashford alionyesha umahiri wake katika mchuano wake wa 150 akiwa na jezi la Man United na kufunga bao katika ushindi mwembamba uwanjani Old Trafford wa 2-1 dhidi ya Brighton.

Ushindi huo una maana kuwa Ole Gunnar Solskjaer ni kocha wa kwanza wa Man United kushinda mechi zake sita za kwanza za ligi. Ulikuwa ushindi wa saba wa United tangu Mnorway huyo alipochukua usukani kwa mkataba wa muda na sasa wako tu nyuma ya Chelsea na pengo la pointi tatu. Paul Pogba aliiweka United kifua mbele baada ya kufunga penalty katika dakika ya 27.

Wakati huo huo, Arsenal walipata ushindi muhimu katika derby kali ya London dhidi ya Chelsea na kujiweka katika nafasi nzuri ya kumaliza katika nne bora.

Ushindi huo umewaweka Arsenal nyuma ya nambari nne Chelsea na pengo la pointi tatu na juu ya United, kwa tofauti ya mabao.

Alexandre Lacazette aliiweka Arsenal kifua mbele ktika dakika ya 14 na mchezo mzuri wa Arsenal ukawawezesha kupata bao la pili na la ushindi kupitia kwa Laurent Koscielny. Vijana wa kocha Mauricio Sarri walijitahidi bila mafanikio huku mkwaju wa Marcos Alonso ukigonga mlingoti katika kipindi cha pili. Lakini hata hivyo walishindwa kutengeneza nafasi za kufunga mabao.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends