Liverpool wabeba taji la EPL baada ya miaka 30, waitandika Chelsea 5-3

Nahodha wa kikosi cha Liverpool Jordan Henderson amenyanyua taji la kwanza la Ligi Kuu nchini England katika dimba tupu la Anfield likiwa taji la kwanza baada ya takribani miaka 30 ya giza kwa Kops hao.

Henderson alipokea taji kutoka kwa Lijendi wa Liverpool Sir Kenny Dalglish ambaye alikuwa kocha wa mwisho kubeba ubingwa huo mwaka 1990 katika sherehe ya kukabidhiwa ubingwa huku wakiitandika Chelsea goli 5-3.

Liverpool walithibishwa kuwa mabingwa wa EPL Juni 25 pale ambapo washindani wa karibu Manchester City walipopoteza mchezo dhidi ya Chelsea ingawa iliwabidi wasubiri mpaka mchezo wa mwisho wa nyumbani kukabidhiwa taji lao.

Wamefanya hivyo mbele ya mashabiki na marafiki zao ambao walipewa ruhusa maalumu ya kuhudhuria mchezo huo katika kuhanikiza ushindi wao.

“Tulisubiri kwa muda mrefu,” alisema Kapteni Henderson ambaye anaendelea kujiuguza kwa majeruhi.

“Kutembea na taji ni historia ambayo haitasahaulika kamwe, tulistahili kubeba taji, asante kwa wanafimilia wenzetu kwa kushuhudia tukio hili kubwa ambalo halijafanyika kwa muda mrefu”. Aliongeza Henderson.

Dimba la Anfield lenye uwezo wa kubeba mashabiki 53,000 lilikuwa tupu tangu Juni 17 ambapo mamlaka ya Uingereza ilitoa taarifa kuwa michezo yote baada kupungua makali ya janga la virusi vya Corona kuchezwa bila mashabiki.

Author: Bruce Amani