Liverpool wasipopewa ubingwa wa EPL itakuwa sio haki – Gundogan

326

Sio sawa, sio haki na haitakuwa sawa kama Liverpool watashindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa sababu tu ya janga la virusi vya Corona (COVID-19) amesema hayo kiungo wa Manchester City Ilkay Gundogan.

Katika kipindi hiki ambacho ligi mbalimbali zimesimama, nchini England hadi angalau mwezi wa nne tarehe 30, Liverpool wanaongoza mbio za ubingwa kwa tofauti ya pengo la pointi 25 dhidi ya bingwa mtetezi Manchester City ambaye wako nafasi ya pili.

Alipoulizwa kama Liverpool wapewe ubingwa wao endapo msimu utafutwa na kushindwa kumalizika, Gudogan aliliambia ZDF kuwa “Kwangu itakuwa sawa.”

“Inatakiwa kama mwanamichezo kutoa haki,” aliongeza staa huyo raia wa Ujerumani.

EPL wanategemea kuwa na kikao tarehe 3 Aprili kujadili juu ya kusogeza mbele zaidi tarehe ya kuanza kuchezwa kwa ligi hiyo huku ikitegemewa kusogezwa mbele kutoka ile tarehe ya awali ambayo ilikuwa Aprili 30.

Itakumbukwa ilipangwa msimu huu kumalizika Mei 17 lakini mpaka sasa hatima ya ligi hiyo ni giza nene kwa kila mmoja kuanzia FA wenyewe mpaka matawi yake

Rais wa Uefa, Aleksander Ceferin, alisema michezo ya msimu wa 2019-20 itafutwa kama itashindwa kuchezwa mwishoni mwa Juni.

Gundogan, 29, aliweka wazi kuwa mamlaka zinazosimamia michezo hivi sasa zinakumbwa na changamoto kubwa kimaamuzi hasa juu ya namna ya kutatua tatizo hilo.

“Kuna maoni tofauti tofauti. Kwa klabu ambazo zimekuwa zikifanya vizuri kufutwa kwa msimu itawaumiza daima, lakini ni ukweli usiopingika kufutwa kwa ligi kwa timu zilizo katika hali mbaya ya kushuka daraja itakuwa habari njema sana kwao,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Dortmund.

Gundogan aliongeza kwa kusema atakuwa tayari kukatwa mashahara wake kama EPL watasema wachezaji na viongozi wakatwe kama Ujerumani kwa Borrusia Dortmund na Bayern Munich wanavyokatwa mishahara yao.

Author: Bruce Amani