Liverpool yaendeleza ubabe Uefa, yaichapa Porto 2-0

Liverpool wameendeleza ubabe wao kwenye mechi za hatua ya makundi kufuzu kucheza 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuvuna ushindi wa goli 2-0 kutoka kwa timu sumbufu ya Porto mtanange uliopigwa dimba la Anfield Jumatano.

Kikosi cha kocha Jurgen Klopp ambacho kabla ya mchezo huo tayari kilikuwa kimejikatia tiketi ya kucheza mtoano baada ya ushindi wa mechi nne za mwanzoni kilianza kwa mabadiliko baadhi ya wachezaji muhimu akiwemo Virgil van Dikj akianzia bechi.

Magoli ya kipindi cha pili ya Liverpool yametosha kumpa furaha Klopp na kuendelea kujiimarisha kileleni mwa kundi kufuatia kiungo mshambuliaji wa Hispania Thiago Alcantara kupiga shuti kali nje ya 18 kabla ya Mohamed Salah pia kumalizia pasi ya Jordan Henderson.

Matokeo hayo yanaifanya Porto kushika nafasi ya pili baada ya AC Milan kushinda bao 1-0 dhidi ya Atletico Madrid, ambapo mchezo wa mwisho utaamua nani ataungana na Liverpool kusonga mbele hatua ya mtoano.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends