Liverpool yatinga fainali ya Champions League kwa kishindo

Liverpool imetinga katika fainali ya Champions League baada ya kufanya maajabu uwanjani Anfield kwa kutoka nyuma na kuilaza Barcelona mabao 4 – 0. Vijana hao wa Klopp sasa wamejikatia tiketi kwa kupata ushindi wa jumla ya magoli 4-3

Baada ya kupoteza kwa magoli 3-0 katika uwanja wa Nou Camp, Liverpool ililipiza kisasi wakati Divock Origi alipoiweka kifua mbele timu hiyo katika dakika ya saba.

Georginio Wijnaldum ambaye aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Andrew Robertson, alifunga magoli mawili katika dakika mbili za kipindi cha pili.

Origi baadaye alifunga goli lake la pili na la nne kwa upande wa Liverpool kutokana na kona iliyopigwa kwa haraka na kukamilisha ushindi huo wa kihistoria.

Liverpool sasa huenda ikacheza dhidi ya Ajax ama Tottenham katika fainali ya mjini Madrid mnamo tarehe mosi mwezi Juni.

Ikumbukwe kuwa Barcelona walicharazwa 3-0 na Roma katika mkondo wa pili wa robo fainali ya kombe hilo mwaka uliopita kutokana na goli la ugenini, baada ya kushinda mkondo wa kwanza 4-1.

Lakini kwa Liverpool ilikuwa kumbukumbu nyengine ya matokeo mazuri ya Ulaya ambayo yanafananishwa na ushindi wao dhidi ya AC Milan katika fainali ya 2005 mjini Istanbul na ushindi wao wa 4-3 dhidi ya Borussia Dortmund katika uwanja wa Anfield miaka mitatu iliopita

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends