Lokosa wa Simba aikacha timu na kutoweka

Uongozi wa Simba, umelazimika kuachana na mshambuliaji wao raia wa Nigeria, Lokosa Junior, baada ya kutoweka kwa siku tatu kwenye mazoezi ya timu hiyo.

Lokosa alijiunga na Simba miezi miwili iliyopita akitokea timu ya Esperance ya Tunisia, aliyokuwa akiitumikia kabla ya kurejea kwao Nigeria ambapo alikuwa nje ya dimba kwa zaidi ya miezi nane.

Simba walimsajili mshambuliaji huyo ikiwa ni sehemu ya kuimarisha kikosi chake hasa baada ya ruhusa ya Shirikisho la Soka barani Afrika CAF, ingawa hajacheza mchezo wowote tangia atue klabuni hapo wa mashindano.

Kwa mjibu wa Blog ya Salehe Jembe inasema kuwa tayari mabosi wa Simba wamevunja mkataba kimyakimya na nyota huyo, jambo lililomfanya ajiondoe rasmi kwenye mazoezi ya timu hiyo akisubiria maslahi yake ya kuvunjwa kwa mkataba huo ili arejee kwao kujipanga na timu nyingine.

“Nimeamini kweli kwenye mpira mchezaji kama akikaa nje ya uwanja kwa muda mrefu, rekodi yake pekee haiwezi kumlinda, maana juzi nilimsikia mazoezini kocha wetu, Gomes (Didier) akimuulizia Lokosa kwa meneja wa timu ambapo alijibiwa kuwa hajafika mazoezini kutokana na kuwa na mazungumzo na mabosi wetu, lakini ukifuatilia mazungumzo nje ya hapo utaona wazi kuwa hatarudi Simba tena.

“Hadi muda huu ninapoongea na wewe ninauhakika kabisa tayari kakatwa kwenye kikosi na yupo njiani kusepa kwao maana ameshindwa kukidhi mahitaji ya timu na vilevile anaonekana kuwa na majeraha sugu yanayomfanya kuwa muoga kugongana hata mazoezini jambo lililomfanya kocha kutompa nafasi ya kucheza,” kilisema chanzo hicho.

Lokosa tangu ajiunge na Simba alicheza mechi moja akitokea benchi dhidi ya TP Mazembe kwenye michuano ya Simba Super Cup.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares