Lukaku atupia mbili, Ubeligiji ikiichapa Estonia 5-2

Romelu Lukaku ameisaidia timu ya taifa ya Ubeligiji kuibuka na ushindi wa goli 5-2 dhidi ya Estonia katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia Qatar 2022, akitupia bao mbili kwenye ushindi huo.

Mabao hayo mawili yanamfanya Lukaku kufikisha goli 66 katika mechi 99 kwenye michuano hiyo ya kimataifa.

Nahodha wa Estonia Mattias Kait alifunga goli la kuongoza kwenye mechi hiyo lakini Hans Vanaken alirudisha bao hilo kwa Ubeligiji ambao bado wanaongoza kwenye viwango vya Fifa.

Lukaku ambaye ni mshambuliaji wa Chelsea akitokea Inter Milan alifunga bao la kwanza upande wake kabla ya kuongeza lingine na kufanya matokeo kuwa 3-1.

Axel Witsel na Thomas Foket walifunga moja moja kabla ya Erik Sorga kupata la kufutia machozi.

Ubeligiji sasa wanaongoza kundi E wakiwa na alama 10 baada ya mechi 4, wakati Jamhuri ya Czech ikiwa nafasi ya pili alama 7, hii ni baada ya kuifunga Belarus 1-0.

Wales hawajacheza mechi ya nne, wana alama tatu pekee.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares