Lwandamina ashinda tuzo ya kocha bora Mwezi Mei

Kocha George Lwandamina wa Azam FC ametwaa tuzo ya kocha bora kunako Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kumshinda Francis Baraza na Abdallah Mohammed.
Lwandamina raia wa Zambia alitwaa tuzo hiyo baada ya kuiongoza Azam kushinda michezo miwili, ambapo ilizifunga KMC mabao 2-1 na Biashara United mabao 2-0 na kuendelea kubaki nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi.
Kocha Lwandamina amefanikiwa kumpiku kocha Baraza wa Kagera Sugar ambaye pia alikuwa na mwezi mzuri na Abdallah Mohamed wa JKT Tanzania.
Makocha waliotwaa tuzo hiyo ni Aristica Cioaba aliyekuwa Azam (Septemba), Cedric Kaze aliyekuwa Yanga (Oktoba), Charles Mkwassa wa Ruvu Shooting (Novemba), Cedrick Kaze, Yanga (Disemba), Francis Baraza aliyekuwa Biashara (Januari), Zuberi Katwila wa Ihefu (Februari), Mohammed Badru wa Gwambina (Machi) na Didier Gomes (Aprili)
Wakati huo huo, Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam, Sikitu Kilakala, kuwa mshindi wa Tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Mei.
Ushindi wa Meneja huyo umefuatia kufanya kwake vizuri katika Menejimenti ya matukio ya michezo iliyofanyika kwenye uwanja huo kwa Mei pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares