Lyon yapinga kufutwa kwa Ligue 1

50

Rais wa klabu ya Lyon inayoshiriki ligi kuu ya Ufaransa Ligue 1 Jean-Michel Aulas ameitaka Mamlaka ya Ufaransa kufikiria upya maamuzi ya kufuta ligi.

Mnano Aprili 28 mamlaka ya Ufaransa ilitangaza kufuta Ligue 1 na Ligue 2 kutokana na uwepo virusi vya Corona.

Lyon wanakamata nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligue 1 jambo lililoiondolea nafasi ya kushiriki mashindano ya Ulaya huku wakiwa wamecheza michezo michache kuliko timu nyingine.

Ligue 1 ni ligi pekee kati ya tano kubwa Ulaya ambayo imefutwa, kwani ligi ya Ujerumani Bundesliga tayari imerudi Mei 16, La Liga, Serie A na EPL zikiwa njiani kurejea baada ya kusimama kwa zaidi ya miezi miwili.

Ligi ya Uholanzi na ligi ya Ubelgiji tayari zimeshafutwa.

“Ligi ya Bundesliga inaendelea hivi sasa, ligi ya Hispania inaendelea Juni 8, Italia, Urusi, na Ureno wameendelea na mazoezi katika kipindi ambacho EPL pia inaelekea kurudi Juni 19”. Alisema Aulas.

“Kwa nini Ufaransa wasifikirie kuirejesha ligi, ni kuishusha hadhi ya Ligue 1”.

“Tunaweza kurekebisha makosa yetu mpaka Juni 2, tuna nafasi hiyo kwenye ligi ya Ufaransa kwa kufuata kanuni za afya, angalau tunaweza kurejesha na kumaliza mwezi Julai au Agosti”. Aliongeza Rais Aulas

Lyon inakuwa klabu ya tatu Ufaransa kuandika mapendekezo ya kuomba ligi irejeshwe tena baada ya Amiens na Toulouse, kuandika maombi yao ya Ligue 1 kurudi.

Author: Bruce Amani