Mabingwa watetezi Gor Mahia waondolewa Sportpesa SuperCup

Wabishi wa Mwanza Mbao FC wamefanya makubwa ya kumuondosha bingwa mtetezi mara mbili mfululizo wa mashindano ya Sportpesa Supercup Gor Mahia katika mchezo uliochezwa katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam kwa njia ya matuta baada ya dakika tisini kumalizika kwa goli 1-1.

Katika mchezo huo Mbao walionekana kuzidiwa kwa kiasi kikubwa magoli yakifungwa na Denis Oliech kwa upande wa Gor Mahia kupitia penati huku goli la kusawazisha likifungwa na Aboubakar Ngalema dakika ya 76 baada ya kupokea pasi mjarabu ya Ally Kombo.

Kipyenga cha mwamuzi kiliashiria kumalizika kwa dakika tisini na Kuruhusu kupigwa kwa penati ambazo zilitamatisha utawala wa Gor Mahia katika mashindano hayo ambapo imefanikiwa kutwaa mara mbili mwaka 2017 na 2018.

Baada ya mchezo huo kocha msaidizi wa kikosi cha Mbao, Ally Bushiri amesema alitambua kasi na ubora wa kikosi cha Gor Mahia hali iliyomfanya awaambie wachezaji wacheze kwa kujiamini bila kuwa na hofu yoyote.

“Niliwaambia wachezaji wajiamini wanaweza kupata matokeo hali iliyowafanya watafute mbinu mbadala za kupata matokeo na hatimaye tumefanikiwa kushinda ni fahari kwetu na taifa,” alisema Bushiri.

Matuta ya Mbao yamefungwa na Said Khamis, Abobakar Ngalema, David Mwasa na nahodha aliyeimaliza Gor Mahia Haroun Shakava huku aliyekosa alikuwa ni Ibrahim Hashimu.
Aidha kwa upande wa Gor Mahia mabao yalifungwa na Francis Kahata, Jacques Tusiyenge na Boniface Omondi huku Shafiq Batambuze na Haroun Shakava wakikosa kwa upande wa Gor Mahia.
Matokeo hayo yameifanya Mbao kufanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo hivyo anamsubiria mshindi kati ya Simba na AFC Leopards

Author: Bruce Amani