Madagascar yajikatia tikiti ya AFCON kwa mara ya kwanza

58

Madagascar imefuzu katika dimba la mataifa ya Kombe la Afrika – AFCON 2019 nchini Cameroon kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo. Bao la Njiva Rakatohatimalala mwenye umri wa miaka 26 anayechezea kandanda lake nchini Thailand liliihakikishia ushindi Madagascar dhidi ya Guinea ya Ikweta.

Matokeo hayo yameiweka Madagascar kileleni mwa Kundi A na pointi kumi na hivyo kujikatia tikiti ya kuelekea Cameroon mwakani.

Senegal watajiunga nao kama watawashinda Sudan. Madagascar sasa ni taifa la 40 tofauti kutinga katika fainali za AFCON.

Kulikuwa na mechi zilizokamilika kwa sare katika kundi B wakati Comoros ilitoka sare ya 2-2 na Morocco na Malawi ikaiteka Cameroon kwa sare tasa

Matokeo hayo yana maana kuwa Cameroon inaongoza kundi hilo na pointi nane, lakini wamefuzu moja kwa moja kama wenyeji  na sasa kuacha nafasi moja tu ya kushindaniwa katika kundi hilo. Morocco ina pointi saba, Malawi ina pointi nne na Comoros ina mbili, huku timu zote zikiwa zimecheza mechi nne.

Katika Kundi C, timu nne zinawania tikiti ya kufuzu, baada ya Gabon kuwalaza wenyeji Sudan Kusini 1-0 na Burundi wakatoka sare ya 1-1 na Mali. Kichapo hicho kina maana Sudan Kusini haina pointi yoyote na haiwezi kufuzu katika AFCON mwakani. Mali inaongoza kundi hilo na pointi nane, moja mbele ya Gabon nayo Burundi ikiwa ya tatu na pointi sita

Katika Kundi H, Guinea na Ivory Coast zinapigiwa upatu kufuzu licha ya timu hizo kutekwa sare katika mechi zao. Ivory Coast ilitoka sare tasa na Jamhuri ya Afrika ya Kati mjini Bangui wakati mjini Kigali, Rwanda ilitoka sare ya 1-1 na Guinea.

Guinea na Ivory Coast zingefuzu zote kama zingeshinda mechi zao za leo. Guinea inaongoza Kundi hilo na pointi 10, Ivory Coast ina saba, Afrika ya Kati ina nne na Rwanda inashika mkia na pointi moja.

Katika Kundi J, Misri iliizaba eSwatini 2-0 na sasa kusogea karibu na kufuzu kwa kujikusanyia pointi tisa. eSwatini haiwezi kufuzu sasa.

Kuna duru mbili za mechi za kufuzu zitakazochezwa Novemba na mechi za mwisho zitachezwa Machi mwakani.

Author: Bruce Amani