Mahakama ya CAS yaahirisha uamuzi kuhusu kesi ya Semenya

107

Mahakama ya Usuluhishi Michezoni – CAS imeahirisha uamuzi wake kuhusu kesi ya Caster Semenya dhidi ya Chama cha Kimataifa cha mashirikisho ya riadha – IAAF hadi mwishoni mwa Aprili.

Bingwa huyo mara mbili wa Olimpiki katika mbio za mita 800 Semenya kutoka Afrika Kusini anataka kubatilisha kanuni mpya za IAAF ambazo zinalenga kupunguza viwango vya homoni za kiume za testosterone katika wanariadha wenye homoni za kupindukia.

IAAF inasema Semenya na wanariadha wengine wa kike ambao wana tofautiana katika hali yao ya kijinsia wanapata faida isiyo ya haki kutokana na viwango vyao vikubwa vya testosterone, lakini katka mbio za kati ya mita 400 na 1,000 pekee.

CAS ilitarajiwa kutangaza uamuzi wake Machi 26, miezi sita kabla ya kuanza Mashindano ya Ubingwa wa Dunia mjini Doha. Imesema kuwa tangu kusikilizwa kwa kesi hiyo Februari 18 -22, pande zote zimewasilisha hoja Zaidi na nyaraka. Hakuna tarehe maalum iliyotangazwa.

Baadhi ya watalaamu wa sayansi wanahoji kuwa kumzuia Semenya kutoka mashindanoni kutokana na viwango vikubwa vya homoni za kiume kutakuwa kama kuwazuiwa wachezaji wa mpira wa kikapu kwa sababu ni warefu sana.

Author: Bruce Amani