Makambo aifikisha Yanga kileleni mapema

Mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu ya Tanzania Young Africans wamepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania baada ya kuibuka na ushindi mwembamba goli 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Pongezi ziende kwa mfungaji wa bao hilo mshambuliaji Heritier Makambo maarufu kama “Makambovic” kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwa ushindi huo wa mchezo wa tatu mfululizo Yanga SC inafikisha pointi tisa sawa na timu ya maafande wa JKT Ruvu wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa licha ya maafande hao kucheza michezo miwili zaidi ya Yanga

Matokeo mengine ya michezo ya hapo jana ni Lipuli FC imechomoza na ushindi wa goli 1 – 0 dhidi ya Allience FC, Mwadui imelazimishwa sare ya goli 1 – 1 na timu ya JKT Tanzania, Mbeya City ikichomoza na ushindi mpana wa magoli 4 – 2 dhidi ya Ruvu Shooting, Ndanda wakiwaduwaza Mtibwa Sugar kwa kuwatandika magoli 2 – 1 Azam wakitota huko Musoma kwa kuvutwa shati na Bainhara United kwa kulazimishwa sare tasa ya bila kufungana

Ligi hiyo inataraji kuendelea tena leo kwa nyasi za viwanja vitatu kutimua vumbi

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Wekundu wa Msimbazi Simba watavaana na Mbao FC katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Tanzania Prisons vs Kagera Sugar na African Lyon watakuwa katika dimba la Uhuru kukabiliana na walima alizeti wa Singida United

Author: Bruce Amani