Makambo asajiliwa na Horoya ya Guinea, Yanga yakachwa

65

Mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo ametimkia Guinea kujiunga na klabu ya Horoya FC ambayo inashiriki ligi Kuu nchini humo.

Taarifa za Makambo kusajiliwa na Horoya zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii mapema leo ambapo timu hiyo imemtambulisha rasmi kama mchezaji wao kwa miaka mitatu.

Makambo ndiye kinara wa mabao katika kikosi cha Yanga msimu huu akitupia kambani mabao 16.

Kulingana na mtandao wa Kalonews, Makambo amesaini mkataba wa miaka mitatu

“Horoya AC imemsajili mshambuliaji kutoka DR Congo Heritier Makambo aliyekuwa akiichezea Young Africans ya Tanzania,” imesema taarifa ya mtandao huo

“Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliyewahi kuichezea Motema Pembe, amefunga mabao 16 kwenye ligi ya Tanzania”

Kwa upande wao Yanga kupitia kwa Mwenyeketi mpya Dr Mshindo Msolla amethibitisha kuwa kweli Makambo na Mwinyi Zahera walienda Guinea baada ya mchezo wetu dhidi ya Ruvu Shooting kujaribu bahati ya kumuuza mchezaji huyo sambamba na kufanya vipimo vya awali.

Ingawa katika hali ya kushangaza mshambuliaji Heritier Makambo ameonekana amevishwa jezi ya timu hiyo licha ya kiasi cha fedha cha usajili kutowekwa bayana.

Kuondoka kwa mshambuliaji huyo ni pigo kwa Yanga ambayo iko kwenye mchakato wa kukiimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao huku kwenye msimamo wa 2018/2019 Makambo amekuwa mhimili wa Yanga kwa kiasi kikubwa.

Author: Asifiwe Mbembela