Makamu wa rais wa FIFA apendekeza mabadiliko katika kalenda ya mwaka kwa sababu ya janga la corona

145

Ligi za Ulaya zinatakiwa kutafakari kubadili misimu izingatie kalenda ya mwaka kutokana na janga la virusi vya corona na kwa kuwa mashindano ya kuwania kombe la dunia la mwaka 2022 yatafanyika mwishoni mwa mwaka, makamu wa rais wa shirikisho la soka ulimwenguni FIFA, Victor Montagliani amependekeza.

“Si wazo la kutupwa kapuni,” Montagliani ameiambia radio Sportiva Jumamosi (02.05.2020). “Linaweza kuwa wazo kwa miaka miwili ijayo na kombe la dunia wakati wa msimu wa baridi.”

Montagliani, raia wa Canada, ni rais wa shirikisho la soka la Amerika Kaskazini na kati na eneo la Caribbean, CONCACAF, ambako misimu ya ligi kubwa za soka na ligi nyingine hufuata kalenda ya mwaka.

Michuano ya kombe la dunia la kandanda 2020 nchini Qatar itachezwa Novemba na Desemba kwa sababu joto kali wakati wa msimu wa kiangazi katika nchi hiyo halitaruhusu mechi kuchezwa katika kipindi cha kawaida cha mwezi Juni na Julai.

Kwa hiyo, kalenda ya kimataifa inahitaji kudurusiwa upya kwa kuwa ligi kubwa na matukio ya michezo kati ya mabara husan Ulaya na Afrika huandaliwa kuanzia mwezi Agosti hadi Mei mwaka unaofuata.

Hatua hiyo ya kudurusu upya misimu mapema yumkini ikazisaidia timu kuendelea na msimu wa sasa kwa njia nzuri, huku ligi nyingi za Ulaya zikiwa zimesitishwa, na nyingine zikiwa zimetangazwa kufika mwisho, kwa sababu ya janga la corona.

Itavipa vilabu hadi mwisho wa mwaka kukamilisha mechi, na mfumo huu ungeweza kuendelezwa bila mabadiliko hadi baada ya kombe la dunia – na pengine baada ya hapo huku rais wa FIFA, Gianni Infantino, akipanga mageuzi makubwa kuanzia mwaka 2024.

“Tulikuwa tayari tumeanza kufikiria kuhusu jinsi ya kuanzisha kalenda mpya kufikia 2024, na sasa kwa janga hili tunahitaji majibu ya haraka,” Montagliani alisema. (DW)

Author: Bruce Amani