Man City wahifadhi ubingwa wa ligi

197

Hatimaye msimu wa kusisimua wa kinyanganyiro cha ubingwa wa Ligi ya Premier umefika tamati. Manchester City wamehifadhi taji la ligi baada ya kuifunga Brighton mabao 4-1 na kujipatia alama 98.

Ushindi huo unamaanisha ngoja ngoja ya Liverpool ya miaka 29 kushinda taji hilo inaendelea, licha ya wao kushinda 2-0 dhidi ya Wolves katika dimba la Anfield.

Ni vigumu kuamini kuwa wakati mwaka 2018 unaisha, Liverpool walikuwa wanaongoza msimamo wa ligi wakiwaacha Manchester City kwa alama tisa.

Mambo kisha yakaanza kwenda mrama na hasa baada ya City na Liverpool kukutana Januari 3 huku Liverpool ikiwa inaongoza ligi kwa alama saba na kuwa na uwezekano wa kujikita kileleni kwa alama 10.

Liverpool hata hivyo walipoteza mchezo huo kwa goli 2-1 na kufanya pengo lipunguwe na kufikia alama nne. Vijana hao wa kocha Jurgen Klopp wamemaliza msimu kwa kupoteza mechi moja pekee na kujikusanyia pointi 97.

Liverpool, maarufu kama majogoo wa jiji hawajanyanyua ubingwa wa Ligi ya England toka mwaka 1990.

Historia inaonekana kutokuwa upande wa Liverpool katika mbio za kuwania ubingwa wa EPL.

Imekuwa ni jambo la kawaida kwa timu ambayo inaongoza EPL wakati wa msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya kuchukua ubingwa.

Author: Bruce Amani