Man City yaibamiza Arsenal na kurejea katika mbio za ligi

Kocha wa Arsenal Unai Emery aliwasili mjini Manchester akiwa na hamu ya kuwekea kikomo rekodi ya msururu wa mechi 11 dhidi ya Pep Guardiola ambayo ilianza tokea siku zao za La Liga.

Lakini baada ya sekunde 48 tu za kipyenga kupulizwa, iliwa dhahiri shahiri kuwa operesheni yake ya kupata ushindi wake wa kwanza dhidi ya Guardiola itasubiri hadi siku nyingine.

Mshambuliaji wa Man City Sergio Aguero aliendeleza mashambulizi yake dhidi ya Arsenal, kwa kufunga hattrick na kufikisha 11 mabao aliyofunga katika nyavu za Arsenal. Bao la Arsenal lilifungwa na Laurent Koscielny lakini wakashindwa kabisa kulivamia lango la wenyeji katika kipindi cha pili.

Mabingwa watetezi City walirejea kwa kishindo baada ya kuduwazwa na Newcastle Jumanne iliyopita. Sasa wako nyuma ya vinara Liverpool na pengo la pointi mbili tu, ambao watacheza Jumatatu usiku dhidi ya West Ham.

“Kitu muhimu ni kuwa tunafahamu tunapaswa kushinda mechi zetu,” alisema Guardiola. “Sisi ni timu nzuri wakati tunapocheza kwa dakika 90. Tunapopnguza kasi, tunashindwa kuwa timu nzuri.”

Arsenal sasa wameanguka katika nafasi ya sita, pointi moja nyuma ya Manchester United ambao walipata ushindi mwembamba wa 1 – 0 dhidi ya Leicester leo Jumapili. Bao la dakika ya tisa la Marcus Rashford liliwapa vijana hao wa kocha Ole Gunnar Solskjaer pointi tatu muhimu.

Solskjaer ambaye ni mchezaji wa zamani wa United anajiimarisha katika nafasi ya kupewa mkataba wa kudumu uwanjani Old Trafford. Ameshinda mechi tisa kati ya 10 katika mashindano yote tangu alipochukua usukani na kulituliza jahazi ambalo tayari lilionekana kuzama mapema msimu huu.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends