Man City yaitandika PSG 2-1 Ligi ya Mabingwa

Manchester City imefanikiwa kutokea nyuma kwa goli moja na kushinda bao 2-1 dhidi ya matajiri wa Jiji la Paris, Paris St-Germain mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi, Kundi A, mtanange uliopigwa dimba la Etihad Jumatano.

Ushindi huo unaifanya Manchester City ambao ji Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England kukata tiketi ya kushiriki hatua ya 16 bora ya ligi hiyo ambayo msimu uliopita waliishia fainali na kupoteza kwa Chelsea.

Katika mechi ambayo ilitawaliwa zaidi na ubora wa Man City, magoli ya timu hiyo yakifungwa na Raheem Sterling ambaye ni bao lake la tatu na Gabriel Jesus akimalizia pasi murua ya Bernando Silva.

PSG walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia kwa winga wa kimataifa wa Ufaransa Kylian Mbappe kunako dakika ya 50 baada ya makosa ya kiulinzi ya Manchester City kushindwa kuokoa vyema mpira wa Lionel Messi.

Matokeo hayo ni kama kisasi kwa City kwa PSG kwani itakumbukwa mchezo wa awali baina ya timu hizo, PSG walishinda bao 2-0.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends