Man City yamnyamazisha Haaland, yaifunga Dortmund 2-1 Ligi ya Mabingwa

Manchester City imeibuka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya Borussia Dortmund mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali raundi ya kwanza, kinda Phil Foden ameweka rekodi ya aina yake.

City walitangulia kujipatia bao la kwanza kupitia kwa kiungo mshambuliaji wa Ubeligiji Kevin de Bruyne akimalizia pasi ya winga wa kimataifa wa Algeria Riyad Mahrez kabla ya kiungo wa Ujerumani Marco Reus kutumia vyema pasi ya Erling Braut Haaland.

Hata hivyo, wakati mchezo huo ukionekana kama utamalizika kwa sare, Phil Foden alikwamisha mpira nyavuni dakika za lala salama akimalizia mpira wa kiungo wa Ujerumani IIlkay Gundogan.

Kipyenga cha mwamuzi kilipulizwa kuashiria tamati ya dakika 90, matokeo yalikuwa upande wa faida wa Manchester City ambao watarudiana na Dortmund wiki ijayo, watakuwa wanahitaji ushindi au sare.

Phil Foden goli alilolifunga linamfanya kuwa mchezaji mdogo kufunga akiwa na umri mdogo kwenye hatua ya robo fainali ya Uefa ingawa anazidiwa na Theo Walcot.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares