Man City yaibomoa Chelsea 6 – 0 na kurejea kileleni kwa kishindo

49

Alipoondolewa uwanjani alipigiwa makofi na mashabiki wote na hata wa kutoka timu pinzani. Sergio Aguero kwa mara nyingine tena aliifungia Manchester City hat trick wakati timu hiyo ikirejea kileleni mwa Ligi ya Premier katika mtindo wa aina yake ilipoisakama Chelsea katika uwanja wa Etihad.

Ushindi wa Liverpool dhidi ya Bournemouth uimaanisha kuwa vijana hao wa Pep Guardiola walihitaji ushindi ili kurejea usukani, licha ya kuwa wamecheza mechi moja ya ziada.

City walifumania nyavu za Chelsea mara nne ndani ya dakika 25 na wakaendelea kuwashambulia Chelsea ambao walipungukiwa maarifa na kudhalilishwa kwa kufungwa mabao sita kwa sifuri. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Chelsea kufungwa sita katika mechi ya Premier katika historia yao.

Raheem Sterling alianzisha karamu ya mabao baada ya dakika nne za mchezo. Sergio Aguero kisha akafunga la pili kabla ya kuongeza la tatu na kuwa mfungaji wa mabao mengi katika historia ya City. Ilkay Gundogan aliongeza la nne katika dakika ya 25 kabla ya Aguero kufunga hat trick yake ya 11 akiwa na City kwa kufunga penalty na kuifikia rekodi iliyowekwa na Allan Shearer. Sterling alifunga lake la pili katika mchezo huo na kuwarudisha City kileleni mwa ligi juu ya Liverpool kwa tofauti kubwa ya mabao.

Katika mechi ya mapema, Tottenham ilihakikisha kuwa inabaki katika kinzanganyiro cha ubingwa baada ya vijana hao wa Mauricio Pochettino kupata ushindi dhidi ya Leicester City uwanjani Wembley. Waliwazaba Leicester 3 – 1 na kuhakikisha kuwa wanasalia katika nafasi ya tatu baada ya mechi 26 lakini wakapunguza mwanya kati yao na Liverpool na City hadi pointi tano. Mabao ya Spurs yalifungwa na Davinson Sanchez, kabla ya Christian Eriksen kufunga la pili. Jamie Vardy aliwafungia Leicester bao la kuwarudisha mchezoni lakini Son Heung-min alihakikisha kuwa wanapata pointi zote tatu katika dakika za majeruhi.

Author: Bruce Amani