Man City yatinga fainali yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, yaibamiza PSG

292

Manchester City imetinga hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuichapa Paris St-Germain mabao 4-1 kwa matokeo ya jumla ya mkondo miwili, wakati Jumanne wakiwapiga matajiri hao wa Paris bao 2-0.

Winga wa kimataifa wa Algeria Riyad Mahrez amefunga magoli yote mawili kwenye mechi ya Jumanne lakini pia alifunga bao moja kwenye mechi ya ugenini Parc Des Princes baada ya lile la Kevin de Bruyne.

Mahrez alifunga goli la kwanza baada ya mlinda mlango kuokoa vibaya shuti kali la de Bruyne kabla ya kufunga ungwe ya pili akimalizia pasi nzuri kutoka kwa Phil Foden.

PSG walihitimisha mchezo huo kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza wakiwa pungufu kufuatia winga wa timu hiyo Angel di Maria kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumfanyia faulo ya makusudi kiungo mkabaji wa Brazil Fernandinho.

Ikiwa kwa sasa kocha Pep Guardiola anahitaji ushindi wa mechi moja kuwa bingwa ila EPL, ameshabeba taji la Carabao, akifanikiwa kubeba Uefa atakuwa ametimiza mataji matatu (treble).

City inakuwa fainali yao ya kwanza kubwa tangia mwaka 1970 ambapo walicheza na Gornik Zabrze na kushinda Kombe la Ulaya.

Manchester City itacheza na mshindi kati ya Chelsea au Real Madrid ambao watakuwa na mchezo Jumatano Mei 5, mkondo wa kwanza ulimalizika kwa sare ya 1-1

Fainali itapigwa Istanbul Uturuki, Mei 29 siku ya Jumamosi

Author: Asifiwe Mbembela