Man United na Varane wafanya mazungumzo ya uhamisho

Manchester United wamefika hatua nzuri ya mazungumzo baina ya klabu ya Real Madrid na wawakilishi wa mlinzi wa kati Raphael Varane kuhusu uhamisho wake kwenda Old Trafford.

 

Mazungumzo baina ya pande hizo tatu yamefanyika kwa kiasi kikubwa kuanzia Ijumaa mpaka Jana Jumapili ingawa inaelezwa kuwa hakuna makubaliano ya kiasi cha fedha pamoja na mkataba.

 

Varane, 28, alishawaambia Real Madrid kuwa hatamani tena kuendelea kukitumikia kikosi hicho ambapo kwa sasa mkataba wake umebakiza mwaka mmoja.

 

Kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer anakusudia kuimarisha eneo la ulinzi kufuatia kukamilisha eneo la ushambuliaji kwa kukamilisha uhamisho wa winga wa England na Borrusia Dortmund Jadon Sancho kwa dau la pauni milioni 73.

 

Varane alijiunga na Real mwaka 2011 akitokea Lens klabu inayoshiriki Ligi Kuu Ufaransa Ligue 1 ambapo kwa kipindi hicho ameshinda mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na La Liga mara tatu.

 

Ni mshindi wa Kombe la Dunia pia mwaka 2018 nchini Urusi, amecheza jumla ya mechi 79 ambapo mwaka 2020 kwenye Euro alicheza mechi zote Ufaransa ikikomea hatua ya 16 bora.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares