Man United wapigwa hadi kuchakaa na Liverpool

Mashetani Wekundu Manchester United wameadhibiwa vikali na mahasimu wao, Liverpool kufuatia kuchabangwa mabao 5-0 jioni ya leo, mtanange uliopigwa Uwanja wa Old Trafford Jijini Manchester.

Mabao ya Liverpool yalianza kufungwa mapema kabisa kupitia kwa Naby Keita dakika ya tano, Diogo Jota dakika ya 13 na Mohamed Salah matatu dakika ya 38, 45, na 50.

Wakati ungwe ya pili, United wakijipanga kujaribu bahati ya mtende kama waliyoipata kwenye mechi dhidi ya Atalanta, kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa Paul Pogba akaonyeshwa kadi nyekundu kwa mchezo usiokuwa wa kiungwana kwa Naby Keita.

Liverpool inafikisha pointi 21 na kusogea tena nafasi ya pili, ikizidiwa pointi moja na Chelsea, wakati Manchester United inabaki na pointi zake 14 katika nafasi ya seba baada ya timu zote kucheza mechi tisa.

Matokeo hayo yanarudisha hofu ya kufutwa kibarua cha kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye amekuwa na wakati mgumu akivuna alama moja katika mechi nne za Ligi Kuu England.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends