Man United yabanwa na kibonde Fulham Old Trafford, mashabiki waongeza Mzuka

154

Manchester United imebanwa mbavu na kibonde wa Ligi Kuu England Fulham kwa kutoa sare ya bao 1-1 mchezo wa Ligi Kuu ya EPL huku Cavani akifunga bao nzuri wakati mashabiki wakijionea mechi hiyo.
Baada ya kuibuka kwa Janga la Virusi vya Corona mwishoni mwa mwaka 2019 hasa mwanzoni mwa mwezi Machi nchini England, mechi zimekuwa zikichezwa bila mashabiki ingawa mwezi Disemba 2020 mashabiki walirudi kwa masharti lakini walizuiliwa tena kutokana na ongezeko la wagonjwa wa Covid-19.
Kukiwa na mashabiki 10,000 ndani ya dimba la Old Trafford mshambuliaji wa kimataifa wa Uruguay Edinson Cavani alifunga bao la kutanguliza kwa Manchester United akimalizia mpira wa kiungo mshambuliaji Bruno Fernandes.
Mara ya mwisho kwa watazamaji kutazama goli kwenye uwanja huo ilikuwa kwenye mechi ya Manchester Derbi ambapo bao la kiungo mkabaji Scott McTominay liliwapa United ushindi.
Bila kuleta changamoto kubwa, United kiurahisi waliruhusu bao la kichwa lililofungwa kwenye dakika ya 76 na Joe Bryan akimalizia pasi ya Bobby Decordova-Reid na kufanya matokeo kuwa sare ambayo hayabadilishi chochote kwa timu zote mbili.

Author: Bruce Amani