Man United yafurushwa na Barcelona ya Messi katika robo fainali

Safari ya Manchester United katika Champions League imefikia kikomo katika robo fainali baada ya Barcelona ikiongozwa na Lionel Messi kuibamiza katika mkondo wa pili uwanjani Nou Camp.

United, ambao walishuka dimbani wakiwa nyuma kwa bao moja kwa sifuri lililofungwa katika mkondo wa kwanza, walianza vyema kabisa mchezo lakini wakaisha pumzi na kuadhibiwa na umahiri wa mchezaji Lionel Messi pamoja na makosa aliyooafanya langoni kipa David de Gea.

Messi aliwaweka wenyeji kifua mbele alipofunga bao maridadi sana kutoka hatua 20 katika dakika ya 16 na dakika nne baadaye De Gea akamwawadia Messi bao la pili kwa kuutema mpira kutokana na shuti la chini chini la Muargentina huyo.

Philippe Coutinho aliongeza la tatu kwa upande wa Barca katika dakika ya 61 kwa kufyatua kombora safi la mbali hadi wavuni

United waligonga mlingoti wa lango katika sekunde 40 za kwanza kupitia Marcus Rashford lakini wakadhibitiwa baada ya kufungwa bao la kwanza.

Ulikuwa usiku wenye kumbukumbu kwa kocha wa United Ole Gunnar Solskjaer kwenye uwanja ambao alifuga bao lake maarufu kabisa, la ushindi katika dakika ya mwisho ya fainali ya Champions League 1999.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends