Man United yakubali yaishe kwa Solskjaer

Kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer anakusudiwa kuondoka klabuni hapo baada ya kuiongoza timu hiyo kuangukia kwenye kipigo cha goli 4-1 dhidi ya Watford katika mchezo wa Ligi uliopigwa Jumamosi Novemba 20.

Hakuna taarifa rasmi ya kuthibitisha kuondoka kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer lakini mabosi wa klabu hiyo wamekutana akiwemo mmiliki Glazers na kujadili hatima ya mtoto wa nyumbani.

Ambapo kwenye kikao hicho, wamejadili kuwa mchezo wa Watford ambao wamepoteza utakuwa wa mwisho kwa kocha Solskjaer ambaye kwenye mechi nane za ameshinda mbili pekee akishika nafasi ya saba.

Mkurugenzi wa Ufundi na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo Darren Fletcher anategemewa kuiongoza timu hiyo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Villarreal Jumanne.

Bado haiko wazi, lakini inaonekana kocha Michael Carrick ambaye alikuwa sehemu ya jopo la kocha Solskjaer ambaye amekutana na vipigo vizito atabakia klabuni hapo.

Uongozi wa United kwa muda sasa wamemvumilia kocha Solskjaer licha ya mara kadhaa kuwa kwenye hali mbaya ya matokeo ukijumlisha na vipigo vya goli 5-0 kutoka kwa Liverpool, 2-0 kutoka kwa Manchester City, kutolewa Kombe la Ligi na West Ham United.

Uvumilivu ambao unaonekana kufikia ukomo hasa wakiangalia namna ambayo kikosi kimekuwa kikishuka kiwango kila kuchwao, kuelekea mchezo wa Uefa mbele ya Villarreal ni rahisi United kwenda kupoteza kama ingeendelea kuamini kwa Ole Gunnar Solskjaer.

Solskjaer alichukua mikoba ya kocha Jose Mourinho kama kocha wa muda mwezi Disemba 2018.

Ambapo alipewa timu jumla mwezi Machi 2019 kwa kandarasi ya miaka mitatu kabla ya kumuongeza mkataba mpya Julai ‪2021-2024‬.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends