Man Utd yafanya usajili wa beki kutoka Crystal Palace

Sasa ni rasmi. Baada ya kuvuja kwa picha zilizomuonyesha mlinzi Wan-Bissaka kusajiliwa na Manchester United kwa siku mbili nyuma sasa imekuwa rasmi leo baada kuthibitishwa na klabu hiyo.

Beki Aaron Wan-Bissaka amejiunga na Manchester United akitokea Crystal Palace kwa dau la pauni milioni 50.

Bissaka ni kinda wa Kiingereza anayekitumikia kikosi cha England cha chini ya miaka-21, alifanyiwa vipimo vya afya siku ya Alhamisi na kutangazwa leo Jumamosi Juni 29 kwa lengo la kufananisha namba ya jezi pamoja na tarehe ya kutambulishwa kwake.

Saini ya Wan-Bissaka inafanya United kufikisha usajili wa pili baada ya ule wa winga Daniel James kutokea Swansea City.

Akizungumzia usajili huo Aaron Wan-Bissaka amesema: “Ni hisia zisizoelezeka kujiita mchezaji wa Manchester United, na kitu ninachokifahamu ni wachezaji wachache sana hupata bahati ya kuichezea klabu kubwa kama hii Dunia”

Bissaka amekabidhiwa jezi namba 29 iliyokuwa ina valiwa na Wilfred Zaha kabla hajaondoka klabuni kwenda Crystal Palace na atakuwa sehemu ya kikosi cha United kinachoingia kambini Julai Mosi.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments