Manchester ni Bluu! City wawakaanga United

Manchester City imerejea kileleni mwa ligi baada ya kuikaanga Manchester United a kupata ushindi wa uhakika wa debi uwanjani Etihad.

Vijana hao wa Pep Guardiola waliingia dimbani wakilenga kupata pointi tatu za kuwarejesha usukani mwa Premier League baada ya ushindi wa Liverpool mapema Jumapili dhidi ya Fulham na mara tu kipyenga kilipulizwa, City walianza kwa kasi na David Silva akawafungia bao.

City walipata la pili baada ya Sergio Aguero kusukuma wavuni kombora kali dakika tatu baada ya kipindi cha pili kuanza.

Vijana wa Jose Mourinho ambao walikuwa bila ya Paul Pogba walipata matumaini wakati Romelu Lukaku kuangushwa na kipa wa City Ederson katika eneo la hatari sekunde chache baada ya kuingia uwanjani kama nguvu mpya. Antony Martial akafunga penalty hiyo.

City hata hivyo walihitimisha kibarua kwa kufunga bao la tatu kupitia Ilkay Guendogan zikiwa zimesalia dakika mbili mechi kukamilika. Bao hilo lilipatikana baada ya wachezaji wa City kubadilishana pasi 44.

City wanaongoza ligi na pointi 32 wakifuatwa na Liverpool na pointi 30 baada ya kuifunga Fulham 2-0 mabao yaliyofungwa na Mohammed Salah na Xherdan Shaqiri.

Chelsea ni ya tatu na ponti 28 baada ya kukabwa sare tasa na Everton ijapokuwa bado inaendeleza rekodi ya kutopoteza mchuano mpaka sasa msimu huu.

Arsenal walihitaji bao la dakika za mwisho mwisho kutoka kwa mchezaji aliyeingia kama nguvu mpya Henrikh Mkhtaryan na kulazimisha sare ya 1-1 na Wolverhampton Wanderers uwanjani Emirates. Hivyo wanafunga tano bora na pointi 24 nyuma ya Tottenham Hotspurs ambao wana pointi 27 baada ya kupata ushindi wa bao moja kwa sifur dhidi ya Crystal Palace Jumamosi.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends