Maneno ya Pep Guardiola Baada ya Kuichabanga Arsenal

216

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amesema ubingwa wa Ligi Kuu England uko mikononi mwao na wakishindwa watakuwa wameshindwa wote.

Guardiola ameyasema hayo baada ya kikosi chake cha Man City kuibuka na ushindi murua wa bao 4-1 dhidi ya vinara wa PL klabu ya Arsenal uliochezwa uwanja wa Etihad Jumatano.

Kwa matokeo hayo ya ushindi, City wanakuwa alama mbili nyuma ya Washika Mtutu wa London ambapo mabao yamefungwa na Kevin de Bruyne mawili, John Stones na Erling Braut Haaland wakati lile la Arsenal likiwekwa kimiani na Rob Holding.

Manchester City mechi tatu zijazo itakuwa dhidi ya Fulham kisha West Ham United na Leeds United ambapo jumla mechi zao zimebakia saba.

“Mbio za ubingwa zipo mikononi mwetu, naamini hatuwezi kupoteza mwelekeo wetu”, alisema Pep Guardiola.

“Hizi mechi tatu zijazo zitatoa picha ya kama tutaenda kule tunakotamani kufika. Lakini ukweli ni kwamba tuko nyuma ya Arsenal”.

Manchester City bado wako kwenye nafasi ya kushinda mataji matatu msimu huu kwani wako nusu fainali Ligi ya Uefa, fainali Kombe la FA na EPL.

 

Author: Bruce Amani