Maoni: Funzo la Tshishimbi katika darasa la Zana Coulibaly

18

Soka ni mchezo wa wazi. Kuchezwa kwa soka sehemu za wazi kunafanya kila mmoja kuutazama mpira katika jicho lake. Ikishafika wakati ambapo kila mtu na jicho lake akamsifia mchezaji au kumkosoa mchezaji fulani, asilimia kubwa huwa ni kweli.

Jicho la dunia linakiri Lionel Messi ni bora, Cristiano Ronaldo ni bora wakati hilo hilo jicho linakiri wachezaji wa aina ya Romelu Lukaku wana kasoro sehemu katika ubora huo, ingawa haiwaondolewi asili ya kufanya vizuri wakijituma.

Hufika wakati katika kuutazama mchezo jicho lako linapingana na mwili katika kutafakari uwezo wa mwanadinga fulani, hata rafiki hupingana, lakini kukubaliana na kutokubaliana huwa sehemu yake.

Katika siku za hivi karibuni dunia ili kataa kuliamini jicho lake lilipomtazama kiungo ‘Kisheti’ Papy Kabamba Tshishimbi akishindwa kutuliza mpira kama zamani, hata mgongeo wake si ule wa Ngao ya Hisani alipocheza dhidi ya Simba kwa mara ya kwanza.

Alikuwa sio Tshishimbi ambaye ana uwezo wa kucheza mpira wa namna zote, mpira wa kistaarabu na ule vijana mtaani huita mpira wa kihuni.

Ulimtazama Tshishimbi alipopangwa dhidi ya Kariobangi Sharks kwenye mashindano ya Sportpesa, mbali na kujiamini, utulivu ulipotea.

Kila shabiki akamtupia lawama, kila mmoja akaona sio yule jicho lake linategemea kumuona hasa likikumbuka ule msimu wa 2017/2018 ambao kweli Papy alikuwa fundi.

Pamoja na kushuka kiwango kwa Tshishimbi kulikoambatana na majeruhi pamoja na kwenda Congo ambako hivi sasa kunaaminika kama si sehemu nzuri wanasoka wanaokipiga Tanzania kwenda huko kutokana na kushuka kiwango wakirudi kutoka huko, kumbuka Heritier Makambo bado jicho langu lilikataa kupepeseka.

Zana Coulibaly, beki wa Simba SC kutokea Ivory Coast

Kukataa kwake kulichangiwa na maneno ya Mubobezi mmoja wa Kimarekani katika kuwajenga na kuwaandaa viongozi bora Bwana Gordon Tredgold ambaye amewai kusema “form is temporary, class is permanent ”

Binadamu tumeumbwa kusahau mambo mapema sana, nilisita kidogo kuamini Tshitshimbi ni “One Season Wonder” nikabakiza akiba ya kile nilichokiona kwa Kabamba ambapo kila mmoja anakinzana na jicho lake kwa ubora alionao.

Imani ya kocha Mwinyi Zahera katika kumpanga Papy inawezekana ilikuwa nguzo kubwa zaidi hasa kwa nchi ambazo hakuna watu wa Saikolojia, Walimu wana kazi bora sana katika kuwajenga wachezaji wa wanapoteza viwango kutokana na matatizo ya ndani na nje ya uwanja.

Baada ya kupondwa na kukanwa na mashabiki wengi na baadhi ya wadau wa soka. Tshishimbi amerudi katika ubora wake, mtazame alipocheza dhidi ya Simba, Namungo, macho yanaweza kukubaliana katika hili kuwa Papy amerudi, kauli rahisi unaweza sema amerudi kuwasuta wakejeli wake.

Funzo kubwa katika hili ni subira, haraka katika kuamua jambo ina poteza vijana wangapi.

Coulibay amejifunza lolote hapa kweli? Tuendelee.

Swali rahisi tu vijana wangapi wamepotea kwa kutoaminiwa? kisha wakazomewa katika mechi tano au sita tu za mwanzo.

Tshishimbi asingekuwa shujaa akisimama kwenye uvuli wa kikosi finyu cha Yanga inawezekana naye angepoteza kiwango chake licha ya kwamba ana class ya juu uwanjani.

Mtazame Zana Coulibay, mtazame Kalius Kindoki, Donald Ngoma na pengine Shaibu Abdalah hawa wasingekuwa mshujaa tungewapoteza walianza vibaya lakini baadae wakaja kuwa tegemeo kwa vilabu vyao.

Hii ndio maana wahenga husema “Subira yavuta heri”

Author: Asifiwe Mbembela