Maoni: Kombe la Mapinduzi Fahari ya Macho

976

Leo nataka kunena mambo kadhaa juu ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea visiwani Zanzibar na namna ambavyo ni fahari katika macho ya watazamaji Tanzania na nje ya mipaka yake. Kama ambavyo wanasema “fimbo ya mbali haiui nyoka”

Malengo ya kuanzishwa kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi pasi na shaka ni mawili. Mosi, ni kusherehesha maadhimisho ya Mapinduzi Matakatifu yaliyofanyika Zanzibar January 12, 1964 ambapo fainali ya michuano hiyo hufanyika siku moja baada ya kilele cha maadhimisho ya Mapinduzi.

Pili, Mashindano ya Mapinduzi yalianzishwa kama sehemu ya kuibua na kukuza michezo visiwani Zanzibar. Malengo yote haya kwa pamoja ndiyo yanajibu swali kinaga ubaga japo msimamo wa swali uko pale pale Kwanini Kombe la Mapinduzi Zanzibar?. Na upi ufahari wake kwa vijana?

Kama majibu yatakua moja ya malengo hayo mawili niliyo yataja.

Mosi, kama lengo ni kusherehesha mbona sherehe za uwanjani haziakisi tukio lenyewe la Mapinduzi?. Hii ni kwa maana mbili. Mosi, Shamla shamla za washabiki uwanjani hazibebi ujumbe wa Mapinduzi Matakatifu. Pili, hamasa ya washabiki kwenda kuchagiza shamla shamla ya mapinduzi ni ndogo sana hata kama viingilio ni vya chini. Hata wale wanaokuwepo unajikuta ni upande mmoja wa klabu za Tanzania Bara.

Pili, kama lengo kuibua na endeleza michezo Zanzibar basi hapa ndo kuna shida zaidi yapaswa kuongeza juhudi zaidi. Hata hivyo mashindano hayo kwa vijana huona fahari na kushiriki mechi moja na wachezaji ambao mara nyingi huonekana kama kioo kwao.

Mathalani, Feisal Salum Fei Toto anaporudi Zanzibar bila shaka vijana wengi huona fahari kuwa karibu naye kijana ambaye wanaona ni zao la karibu na maskani yao.

Mosi, Kombe la Mapinduzi limepewa thamani ndogo sana kwa bingwa wa michuano hiyo jambo ambalo inapelekea kuonekana michuano ya kawaida japokuwa kuna timu kubwa zinazoshiriki kwenye michuano hiyo kama klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara kama vile Simba Sc, Yanga Sc, Azam Fc na Namungo Fc.

Kwa mfano, msimu uliopita 2021 bingwa wa Mapinduzi Cup Yanga Sc walivuta mpunga wa hela ya kitanzania Milioni 15 ambazo vijana wa mjini hufananisha michuano hiyo kama Ligi za mchangani.

Pili, Kuna haja kubwa sana ya kuongeza timu zenye upinzani. Hapa ningeomba nieleweke vizuri, kumbu kumbu zinaonesha mara ya mwisho kwa timu za Zanzibar kuchukua ubingwa wa michuano hiyo ni mwaka 2009 ambapo timu ya Mlandege ilifanikiwa kunyakua kombe hilo na KMKM kushika nafasi ya pili.

Sasa hapa nachotaka kuzungumzia upinzani hasa kwa timu za visiwani Zanzibar zinaonekana kuwa timu za kawaida mbele ya timu za Tanzania bara. Ndiyo uchumi mdogo, ushindani mdogo lakini sidhani kama haja ya mashindano ni utawala kuwa wa upande mmoja.

Tatu, Kiu kubwa za Wazanzibar ni kuona timu na wachezaji wanaocheza kwenye Ligi ya Tanzania Bara. Hapa huenda kuna kitu cha kujifunza kwa Mamlaka za michezo Zanzibar ikiwemo uboreshaji wa ligi za ndani sambamba na kuongeza thamani ya ligi hizo.

Mwisho, Kombe Mapinduzi kama litapewa nguvu ya uwekezaji ni miongoni mwa mashindano ambayo yangeendelea kuvuta hisia na kudumisha historia kutokana na jinsi ambavyo linafuatiliwa kuanzia kwenye runinga na hata uwanjani wakati timu zikicheza.

Hivyo “Over To You” Mamlaka za Michezo Zanzibar kukuza au kuacha Mapinduzi Cup kuitwa ‘ Kombe la Pweza’.

Author: Asifiwe Mbembela