Kwa nini EPL wanataka kulazimisha kumalizika kwa ligi hiyo

Ligi Kuu ya England (EPL) imejipanga kuhakikisha inamaliza mechi zote zilizobakia ili kuondoa sintofahamu inayoendelea juu ya hatima ya ligi hiyo.

Katika kuhakikisha ligi inamalizika mapema, EPL imeandaa kikao kitakachofanyika kwa njia ya simu na bodi ya ligi ambapo kikao hicho kitafanyika leo Alhamis.

Michezo yote imehairishwa mpaka Aprili 4 kutokana na hofu ya Virusi vya Corona ambavyo vimeleta changamoto katika mashindano tofauti tofauti duniani, licha ya tarehe hiyo kupangwa bado hakuna uhakika kama virusi hivyo vitakuwa vimepatiwa ufumbuzi.

Kusitishwa kwa michuano ya Euro 2020 kumeipa mwanya mpana EPL kumalizika hata mwishoni mwa mwezi Juni.

Aidha, bado vilabu havijapewa tarehe maalumu ambayo mechi zilizosimamishwa zitaendelea na swali kubwa ni kuwa lini taifa la Uingereza litatoa ruhusa ya mikusanyiko ya watu huku kukiwa na taarifa kuwa hata kama UK hawaruhusu mikusanyiko bado FA wataruhusu michezo hiyo kuendelea bila mashabiki ila kulazimisha kumalizika kwa ligi hiyo.

UNAWEZA KUJIULIZA KWA NINI WANALAZIMIKA KUMALIZA LIGI KABLA YA MWEZI JUNI, HIZI NI BAADHI YA SABABU.

Mosi, EPL italazimika kuendelea hata bila mashabiki ili kutoleta hasara ndani ya Shirikisho hilo kupitia wadhamini na wadau mbalimbali wa ligi hiyo. Kwa mfano endapo ligi itafutwa moja kwa moja EPL watatakiwa kulipa fidia ya zaidi ya pauni bilioni 3 kwa kampuni ya BT Sport na SKY. Ukitazama hilo unaona namna ambayo itakuwa vigumu ligi kutomalizika.

Kauli ya Mkurugenzi wa michezo wa Brighton Hove Albion Bwana Paul Barber imeongeza uzito wa ligi kumalizika ambapo amesema itakuwa sio haki kwa vinara Liverpool kama ligi haitamalizika na kuwakosesha ubingwa ambao wameongoza kwa muda mrefu.

Tatu, vilabu vinavyoongoza kwenye ligi daraja la kwanza vimesema vitafungua madai mahakamani kudai haki yao ya kupanda daraja na kucheza ligi kuu. Vilabu hivi vinao kuwa kufutwa kwa ligi kuzinyima fursa ya kupanda daraja.

Mikataba ya wachezaji ni kipengele kingine kinachovuta hisia za wengi kuwa itakuwaje endapo ligi itaenda hadi Juni au zaidi lakini pia ligi ikifutwa itakuwaje. Kuna wachezaji ambao mikataba yao inaisha mwanzoni mwa mwezi Juni lakini kuna inaoisha mwishoni mwa mwezi Juni pia kuna wengine wameongezewa msimu mpya yote haya yanaleta ugumu wa msimu kufutwa.

Yote haya yanategemewa kujadiliwa katika kikao kilichopangwa kufanyika leo Alhamis ingawa tunafahamu kuwa itakuwa vigumu ligi kutomalizika kwa sababu italeta hasara kubwa kwa Shirikisho lakini pia kuna mikataba italeta changamoto katika kumalizika kwake.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments