Maoni: Nimlaumu nani, TFF, Bodi ya Ligi, Azam TV au Waamuzi
Ni kitendawili kigumu, nashindwa kukitegua. Kitendawiliii…? Nakumbuka wakati ningali kijana mdogo niliwahi kuulizwa kuwa ‘ kati ya kamba na hewa kipi kinavutwa?’. Swali hili lilinifanya nitafakari sana juu ya usahihi wa jibu lake.
Wakati nahangaika kutafuta jibu la swali hili najikuta nipo kwenye dimbwi la maswali lukuki juu ya soka letu la Tanzania. Swali kubwa je, nani nimlaumu, TFF, Bodi ya ligi, Azam TV au Waamuzi?
Ugumu wa swali hili linakuja baada ya matukio mbalimbali ambayo nakutana nayo wakati nautazama mchezo wangu pendwa wa Mpira wa miguu. Any way, ngoja nianze hivi..
Mnamo tarehe 20 Novemba mwaka huu sikua miongoni mwa watu ambao walihudhuria kwenye Uwanja wa Ilulu Ruanga, kuutazama mchezo kati ya Namungo FC na Yanga SC lakini niliushuhudia mchezo huo kupitia Runinga. Wakati naendelea kutazama mchezo huku nikishushia kahawa, dakika ya 78′ lilitokea tukio ambalo lilipelekea penati.
Wakati natafakari juu ya tukio hilo napata kigugumizi nikijiuliza kweli tukio lile lilipaswa kuwa penati? Ilinichukua muda kulitazama kwa makini ndipo akili yangu ikapata jibu na kujisemea moyoni kuwa Mwamuzi wa mchezo anapaswa kulaumiwa juu ya tukio lile kwani marudio ya picha yanaonesha haikuwa penati kupewa klabu ya Yanga, hata kama watoto wa mjini wanasema penati laini bila shaka ile si miongoni mwa hizo laini.
Labda pengine macho yangu yanamakengeza hayakuona vizuri kwenye tukio lile la Yanga sasa hata matukio yale ya kwenye mechi ya Simba dhidi ya Namungo? Hapa sizungumzii kadi nyekudu iliyotoka kwa Namungo Fc au labda ile faulo aliyochezewa Kibu Denis hapa nazungumzia mwenendo mzima wa mechi yenyewe.
Katika mchezo ule kadi nyingi zilienda kwa upande wa Namungo Fc, si kosa hata kidogo, la hasha kisaikolojia ya mchezo mchezaji anakuwa hayupo mchezoni pale damu ikichemka.
Lakini wakati nikilaumu Waamuzi najikuta bado nipo gizani kwa maana hata nikiwa najaribu kupitia baadhi ya picha za marereo hazioneshi vizuri muonekano wa matukio yenyewe hapo ndipo najikuta nawaza ingekuwaje kama tungekuwa na vifaa bora kama wenzetu.
Kuna muda unatazama tukio nzito, lililotoa maamuzi mazito kimatokeo lakini unakosa maamuzi sahihi katika ukirejea kulitazama tukio hilo mara 20.
Kama utakubaliana na mimi kwenye mechi ya Yanga vs Mbeya Kwanza kuna baadhi ya matukio hayaonekani vizuri na kupata tafsiri mfano mchezo wa Yanga na Biashara United tukio la kuangushwa kwa Jesus Moloko na kupelekea penati halipo wazi.
Inawezekana kweli waamuzi wanashida lakini si ajabu linaweza kuwa tatizo moja kati ya mengine ambayo yanarudisha nyuma kandanda ya Tanzania, hapo ndipo najikuta katika wimbi la kuuliza nani anyoshewe kidole.
Japo nimefuta akilini lawama zote hizo kwa Waamuzi na Azam Tv kama mrusha matangazo ya Runinga je na haya nayo vipi?
Matukio yote hayo wanayotokea uwanjani huwa yanafanyiwa tathimini na tutolewa ufafanuzi na TFF kama mzazi wa mpira Tanzania pamoja na Bodi ya Ligi kama msimamizi. Lakini nabaki bumbuwazi pale ninapoona matukio kama hayo yanajirudia msimu mzima na hata yale ambayo hutolewa adhabu ama onyo huwa bado yanaendelea vile vile. Sasa najiuliza sheria na kanuni zetu hazina meno au sheria zetu nyepesi kiasi ambacho hata kosa likifanyika huwezi jutia.
Ngoja nitupe kalamu kwa kusema hili. Pengine kitendawili changu kitateguka kwa kila upande kuwa waadilifu. Warusha matangazo kwenye Runinga yaani Azam Tv wajitahidi kuongeza vifaa ili tuweze kupata picha ya kila kona, na upande wa Waamuzi ni vema kusimama kwenye maadili ya taaluma ya uamuzi, kutupilia mbali mapenzi na ushabiki au presha ya mchezo husika.
Lakini kwa upande wa Tff na Bodi ya Ligi wajikite katika kusimamia vizuri sheria, kuzipitia na kuziboresha ili ziendane na wakati tuliopo. Semina na mafunzo kwa Waamuzi nadhani ndo dawa pekee ambayo inaweza kutibu homa za lawama kwa waamuzi wetu.
