Maoni: Simba Ajibu wa nini, Azam Watampata Lini?

529

Labda wahenga waongope, lakini Simba SC wanasema Ajibu wa nini, Azam waliwaza watampata lini?’. Au ule usemi wa nguo chakavu ndio dekio jipya ufutwe. Ila ni wazi kuwa utumwa wa Ajibu Simba sasa anaweza kuwa mfalme kwenye ngome ya wana lambalamba wa Azam Fc.

Ibrahimu Ajibu Migomba ‘Cadabra’ ndivyo ajulikanavyo kwenye ulimwengu wa kandanda Tanzania. Alianza kusakata kabumbu kwenye Ligi Kuu Tanzania mnamo mwaka 2013 akitokea Simba B. Nyota yake ya ufalme wa soka Tanzania ulianzia Jangwani baada ya kuleta neema ya mvua ya magoli kwenye klabu ya Yanga Sc. Kitakwimu Ajibu akiwa Yanga alicheza mechi 59 na kuweka wavuni mabao 14 akiwa na assisti 22 katika msimu wa 2017/2018 kabla ya kutimkia tena Msimbazi mwaka 2019.

Ufalme wa Ibrahimu Ajibu Migomba katika klabu ya Simba haukuonekana tena kutokana na uwepo wa mafundi wa kabumbu akiwemo kiungo kutokea Lusaka, Zambia Clatous Chotta Chama, Rally Bwalya, Luis Jose Miquissone na wengine wengi.

Ni hivi, Ibrahimu Ajibu japo alikuwa fundi wa kuchezea mpira atakavyo na uwezo wake wa kuichezesha timu na uhodari wa kupiga mipira nje ya 18 lakini bado Mwalimu huyu akiingia na kutoka kauli ni ile ile kuwa mchezaji huyu akiongeza bidii ni mwenye kiwango cha juu kabisa. Lakini tangia hapo kujituma huenda hakupo hata nafasi pia haikuwepo kabla ya kwenda Azam Fc.

Akiwa Msimbazi Ajibu alicheza mechi moja msimu wa 2021/22 na kufunga goli 1 na akitoa asisti moja. Ule uhodari wake ulitetea ghafla na kukosa nafasi kabisa katika klabu ya Simba ambapo watu wengi huamini kama angepata nafasi huenda angerudisha ufalme wake.

Kabla ya kutua Chamazi mechi yake ya mwisho kucheza akiwa na klabu ya Simba ni mchezo kati ya Simba na Namungo na kuonesha kiwango kizuri na kufanikiwa kutoka na assisti moja ndani ya dakika 15′ alizoaminiwa.

Ufalme wa Ajibu utarudi hivi pale Chamazi..

Kiufundi, Ibrahimu Ajibu Migomba (Cadabra) ni kiungo mshambuliaji anatumia sana mguu wa kulia pia anauwezo wa kuutumia vizuri mguu wa kushoto. Ni mtalaamu wa kupiga chenga na anauwezo wa kupenyesha pasi sehemu hatarishi kulia, kushoto na katikati.

Unaweza ukakadiria moja kwa moja kuwa atakuwa na wakati bora. Kutokana na uwezo wake wa kufanya maamuzi, kwa muda gani timu ishambulie na muda gani timu ichezee mpira kunaweza kukawa na faida kwa klabu ya Azam Fc katika eneo la kati kati na mwisho ambalo ndio eneo lenye mapungufu kidogo kwa Azam Fc.

Kuondoka kwa Aboubakari Sure Boy kwenye kikosi cha Azam kunaweza kumfanya Ibrahimu Ajibu kujihakikishia namba na kuonesha njonjo zake ambazo zinaweza kumfanya kuwa Mfalme wa Chamazi.

Ukichukua rekodi ya Ajibu akiwa Yanga na ukiangalia na uwezo wake aliouonesha Simba hivi karibuni ni wazi kuwa Ajibu ni mchezaji mzuri mwenye kipaji na hakika ataweza kurudisha heshima yake akipata nafasi pale Chamazi.

Uwepo wake katika klabu ya Azam itanufaika na uwezo wake wa kutoa assist kwenye eneo la mwisho, uwezo wake wa kukaa na mpira wakati timu inakwenda kushambulia na uwezo wake wa kupiga mipira ya mbali kutakuwa na faida kubwa kwa klabu.

Ni hivi, kuwa si chochote kwenye eneo fulani haimaanishi kama hujui kuna mambo mawili. Mosi huenda uwepo wako katika eneo hilo haukuuthamini na kuweza kuwaonesha kile ulichobalikiwa. Pili, huenda sehemu uliopo kuna wajuzi zaidi yako ambapo unatakiwa kuonesha ujuzi zaidi na kujifunza zaidi ili kufikia daraja la wale ambao wamekuzidi. Kama kweli Ajibu hana tabia ya kupenda kujituma mazoezini basi chochote kinaweza kutokea lakini kupitia uwezo wake alionao, Ajibu atakuwa dhahabu iliyokuwa matopeni pale Chamazi.

Author: Asifiwe Mbembela