Maoni: Simba Ya Chama Na Sakho Moto Zaidi Ya Ile Ya Miquissone?
Watu wengi wanajiuliza Simba ya Chama na Sakho itakuwaje? Nilipata wasaa wa kukutana na wapenzi na mashabiki wa Simba wakiwa wanabishana kwenye vijiwe vya kahawa kuwa Simba ya Chama na Miquissone ilikuwa moto na wengine wanasema Simba ya Chama na Sakho itakuwa ya moto zaidi ya ile.
Kiufundi, Chama ni kiungo mchezeshaji mwenye uwezo mkubwa wa kukaa na mpira, kupiga chenga, kutoa pasi za mwisho na mnyumbulifu na mbunifu hasa pale timu inapoenda kushambulia. Anauwezo mkubwa wa kuammua muda gani timu ishambulie na muda gani timu ichezee mpira.
Luis Jose Miquissone kiufundi ni winga mshambuliaji anaetokea hasa kushoto, mjanja kama sungura mwenye kasi na nguvu haswa.
Muunganiko wa Chama na Miquissone wakati wakiwa Simba Sc ilikua hatari sana. Unyumbulifu wao uliisaidia sana Simba kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu na Kimataifa.
Ki takwimu katika mabao 78 ambayo Simba walifunga msimu uliopita wachezaji Clatous Chota Chama na Luis Miquissone walihusika kwenye mabao 42 yaliyofungwa na klabu ya Simba msimu uliopita.
Clatous Chota Chama amehusika kwenye mabao 23 (kufunga na asisti) wakati Luis Miquissone alihusika katika mabao 19 (kufunga na asisti).
Kwa kuiweka sawa, Chama na Miquissone walikuwa na mchango wa asilimia 53.85 ya mabao ya Simba msimu uliopita.
Twende sawa, kwa takwimu hizo utaona namna gani simba ya Chama na Miquissone ilikua moto.
Ngoja nikwambie kitu…
Simba ya Chama na Sakho itakuwa moto zaidi ya ile ya Miquissone hii ni kutokana na uwezo mkubwa ambao anaonesha Pape Ousssmane Sakho hivi katibuni.
Kutokana na uwezo wake na majukumu ambayo kocha humpatia hasa pale anapocheza kama mshambuliaji huru anakua hatari zaidi.
Mabeki wa timu pinzani wanashindwa kupata mbinu mzuri ya kumzuia hivyo itafanya mabeki wa timu pinzani kulazimika kuwa makini sana kwake na kuwaacha washambuliaji wengine kama Medie Kagere ambaye hana mzaha kwenye kuzisalimia nyavu.
Wakati nikiwaza hilo nakumbuka kuwa kumbe Simba ya Chama na Miquissone ulikuwa uhalisia lakini Simba na Sakho bado ni ndoto za tetesi katika soka la bongo.
