Maoni: Songombingo ya Waamuzi Yaendelea NBC League
Miongoni mwa mambo yanayoibua malalamiko kwenye kabumbu ni juu ya sheria namba 11 ya kuotea ‘Offside’. Iwe umeisoma au vinginevyo, bado kumekuwa na utofauti hasa kwenye tafsiri yake, hapa ndipo napata swali “Je, tatizo ni waamuzi wetu au sheria yenyewe ya Offside?”.
Kuotea ni mchezaji kuzidi au kupokea mpira akiwa mbele ya mchezaji wa pili kutoka eneo la pili la uwanja ambapo hufaidika na kuupokea mpira kwenye eneo hilo. Eneo la kuotea huanza kuhesabiwa kuanzia kwenye mstari wa katikati ya uwanja.
Mchezaji atakuwa ameotea iwapo mpira utapigwa golini na kugonga mlingoti mmoja wapo wa goli au mlinda mlango na kurudi ndani ya uwanja na kuguswa na mchezaji aliyekuwa katika nafasi ya kuotea.
Ikiwa mchezaji yupo katika nafasi ya kuotea na mwenzake mwenye mpira akapiga mpira golini moja kwa moja bila kumpasia mpira huyo aliyeko katika nafasi ya kuotea na kufunga goli, hapo mwamuzi ataruhusu goli bila kutafsiri kuotea.
Aidha, hakutakuwa na dhana ya kuotea pale mchezaji atakapokutana na mpira uliochezwa na mlinda mlango.
Mchezaji akiwa kwenye eneo la kuotea hatohesabika kama kaotea endapo hatojishughulisha kabisa na mpira. Kujihusisha inaweza ikawa kutishia pekee au kuugusa mpira.
Labda nianze kwa upande wa sheria huenda kuna baadhi ya vipengele vingeweza kurekebishwa ili kupunguza malalamiko ikiwemo pale mchezaji yupo katika eneo la kuotea na hatojishughulisha kabisa na mpira. Nahisi hili pengine waamuzi wetu wanashindwa kutafsiri vizuri maaana ya kutojishughulisha na mpira.
Ukija upande wa waamuzi utajua kuna makosa mengi sana wanayafanya ambayo hayahitaji mjadala jadidi. Mfano mtanange baina ya Biashara na Coastal Union, Yanga dhidi ya Mbeya City na Simba dhidi ya Mbeya kwanza. Hapo sijazungumzia matukio mbali mbali yaliyowanyima Azam FC penati zaidi ya tano kwenye mechi tofauti. Hapa kuna kitu cha kujiuliza na hasa ni vitatu.
Mosi, Juu ya kiwango cha weledi wa waamuzi wetu. Nadhani kuna tija ya kuendelea kuwafanyia semina na mafunzo ya mara kwa mara waamuzi wetu sababu kuna wakati inaonesha kana kwamba waamuzi wetu hawajui baadhi ya vitu (hasa kwenye kutafsiri), sio Tanzania tu, tumeona makosa ya waamuzi kwenye michuano ya AFCON 2021 hadi Ulaya.
Mathalani kwenye mechi ya Yanga SC vs Mbeya City kuna maamuzi mengi yalipendelea upande wa Mbeya city lakini unajiuliza je kweli Mbeya city wanaweza kumnunua mwamuzi mbele ya Yanga?, hapana.
Tatu, Mapenzi binafsi ya waamuzi. Ni kweli kinachotafuna waamuzi wetu ni uadilifu na mapenzi yao, kuwa na mapenzi na timu A siyo dhambi kama utaweza kuweka kando mapenzi na kuruhusu weledi kufanya kazi. Kama mahaba na timu B au A yatakufanya kushindwa kutimiza wajibu wako hapo lazima kidole kitanyoshwa.
Mwisho wa hayo yote ni Uadilifu, Semina na kuwepo kwa VAR. Kwa Tanzania nadhani ni wakati sasa kuanza kutumia VAR ingawa hata ya kivyetuvyetu maana ile yenyewe ni gharama lakini pia hatujafikia mazingira salama na wezeshe. Kuwepo tu hata kwa runinga uwanjani ambayo itakuwa inarejesha matukio kwa mjongeo tofauti inaweza kupunguza malalamiko kwa timu na mashabiki.
Ni wakati umefika wa kupunguza machungu na kuokoa hasara za timu ambazo huenda zisingeshuka daraja kama tu zisingedhulumiwa alama zao kutokana na maauzi yenye dosari, Waziri wa Fedha na Mfadhili wa zamani wa Singida United Mwiguli Nchemba amesema ataongea na Waziri wa Michezo juu ya kupatikana kwa VAR inawezekana aliandika kimasihala lakini inaweza kuwa na suhulu zaidi.
