Mashabiki wanataka Loew aondoke baada ya maangamizi ya nchini Uhispania

Licha ya Chama cha Soka nchini Ujerumani DFB kusema kuwa hakitamtimua Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Joachim Low, mashabiki na baadhi ya mastaa wa zamani wa timu hiyo wanataka kocha huyu abwage manyanga mwenyewe kama hatopigwa kalamu. Hilo linakuja ikiwa ni siku mbili tangu kikosi cha Ujerumani kupigwa kipigo cha mbwa mwitu na timu ya taifa ya Uhispania goli 6-0 katika mchezo wa Ligi ya Mataifa Ulaya uliopigwa Jumanne mjini Sevilla.

Mashabiki wamepanga kumuonyesha kadi nyekundu kocha huyo ikiwa ni ishara ya kutomtaka sambamba na baadhi ya wachezaji wa zamani wa timu hiyo wakidai ameiabisha timu yao. Mashabiki wamechukia zaidi kwa sababu ni kipigo kizito zaidi katika historia ya timu hiyo kwani mara ya mwisho kufungwa magoli sita ilikuwa mwaja 1931 katika mtanange wa kirafiki dhidi ya Austria.

Loew alifanya kikao na Rais wa DFB Fritz Keller Jumatano mjini Munich huku kukiwa kumesalia muda wa miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa huenda akaendelea kuwa na kikosi hicho kwenye mashindano ya Kombe la Ulaya mwakani mwezi Juni.

Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la SID ambalo ni tawi la shirika la habari la AFP, asilimia 84.0 ya mashabiki nchini Ujerumani wanataka kocha huyo kufutwa kazi na Mkurugenzi wa Michezo Oliver Bierhoff pia kuachia madaraka

Wakati huo huo asilimia 13.3 pekee wanataka kocha na Mkurugenzi wa Michezo waendelee kubakia pamoja kwani walishashinda Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.

Hata hivyo huenda taarifa hizi zikawa chungu kwa Liverpool na Bayern Munich ambao huenda mmoja wapo akashuhudia kocha wake akienda kuchukua mikoba ya kocha Low endapo mamlaka nchini Ujerumani zitaamua kuachana na Mwalimu wao wa sasa.

Lothar Matthaeus, ambaye alikuwa nahodha wa Ujerumani mwaka 1990 alisema Low lazima aache wazi nafasi ya ukocha kwa wenzake. Baada ya kukinoa kikosi cha Ujerumani kwa miaka 14 inaonekana kocha Joachim Low ushawishi ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo, kujiamini kwake kumepungua mara dufu alisema Matthaeus.

Sare ya 3-3 dhidi ya Switzerland ilikuwa ishara tosha kuwa kocha huyo amepoteza uwezo wake wa awali lakini mechi ya Hispania pengine ndiyo iliyotazamwa zaidi. Kiungo wa zamani wa Liverpool na Ujerumani  Dietmar Hamann amesema Low anakosa mchezaji kiongozi katika timu yake ya hivi sasa.

“Mara zote tulikuwa tumezoea timu yake ikiwa bora, wachezaji bora ambao walikuwa na uwezo wa kumaliza shida zao na tofauti zao ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo lakini saizi anakosa msaada huo” alisema Homann.

“Inaonekana saizi anashindwa kuifikisha timu hata kwenye matarajio madogo kama ambavyo ilikuwa miaka mitatu iliyopita”. Hamann anasema DFB lazima ikubali kubeba msalaba huu kwani kosa kubwa lilikuwa la kumpa mkataba mpya baada ya kushindwa kuonyesha makali kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi..

Author: Bruce Amani