Masoud Djuma aondoka Simba

Aliyekuwa kocha msaidizi wa wekundu wa Msimbazi Simba SC Masoud Djuma Irambona, huduma yake imefikia kikomo baada ya uongozi wa klabu hiyo ambayo ni mabingwa wa soka Tanzania kusitisha mkataba wake katika kile umesema kuwa ni kuweka hali shwari katika benchi la ufundi ambalo liliripotiwa kwa miezi kadhaa kwamba halina maelewano kati yao.

Djuma kipenzi cha mashabiki ameondoka huku akionyesha bado anakiu ya kufanya kazi klabu hapo lakini mgogoro kati yake na kocha mkuu Patrick Aussems umewafanya wawili hao wameshindwa kula sahani moja

Kaimu Rais wa Wekundu wa Msimbazi Salim Abdallah maarufu kama “Try again” akizungumza juu ya hatima ya kocha huyo, amesema kocha huyo msaidizi alikua na matatizo mengi hasa na makocha wakuu wa timu hiyo, tabia ambayo uongozi wa timu hiyo umeshindwa kuvumilia “kumekua na matatizo yanayojirudia rudia kati ya Djuma na benchi la ufundi hasa makocha wakuu, licha ya kufanya jitihada za kumaliza matatizo hayo siwezi kueleza mengi zaidi tutakuja na tamko rasmi”

Kocha huyo kijana alipotua tu katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Oktoba 2017, alikuja na kutoa Kauli mbili za kuwa hatafunga begi lake na kama mabaya ataondoka zake mapema kurejea Kigali Rwanda, na pia alisema wachezaji wavivu wajiandae, kauli hiyo iliwavutia sana mashabiki wa klabu hiyo na kuona sasa wamepata mwalimu anayestahili kufanya kazi hapo Msimbazi

Kutokana na wengi kuvutiwa na kauli hiyo, wamekuwa wakijadili mambo kadhaa ikiwemo kuwachambua wachezaji wavivu na wasiojituma mazoezini na katika mechi kitu kinachosababisha kwa timu hiyo kufanya vibaya.

Mbinu yake ya kutoa maelekezo kwa wachezaji mizuka pale timu yake inaposhambulia na hata inapokosa goli aina ya ushangiliaji wake, wapenzi na masahaibiki wa soka hasa wa klabu ya Simba iliwavutia sana na akafananishwa na ile ya kocha wa Manchester City ya England Pep Guardiola.

Masoud alikua karibu sana na wachezaji pia na mashabiki wa timu hiyo kitu kilichopelekea kupendwa mno na mashabiki hao. Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakieleza kufurahishwa na namna kocha huyo alivyoonyesha kujiamini huku baadhi wakitaka viongozi na wachezaji wenyewe kumuunga mkono. Dalili za Masoud kuondolewa Simba zilianza kuonekana tangu mwezi Septemba baada ya kuachwa kwenye safari ya mechi za mikoani, Mtwara, Mwanza na Shinyanga ambako timu ilishinda mechi moja tu 3-1 dhidi ya Mwadui FC, nyingine mbili ikitoa sare ya 0-0 na Ndanda FC na kufungwa 1-0 na Mbao FC.

Lakini wadau wa michezo walipotaka kufahamu sababu kubwa ya kocha huyo kuachwa katika msafara wa michezo ya mikoani kitu ambacho si kawaida kwa wekundu hao wa Msimbazi, majibu ya uongozi wa juu wa Simba walisema Masoud ana shughuli nyingine za klabu alizopangiwa kufanya ikiwemo kuwachunguza wapinzani wa Simba SC katika mechi zijazo na kusimamia mazoezi kwa wachezaji wa kikosi cha pili cha timu hiyo.

Na alipoibuka benchi wakati wa mechi dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa sare ya 0-0 Jumapili iliyopita Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam imani ikarejea kwamba atabaki. Juma aliwasili nchini Oktoba 19, mwaka jana akitokea Rwanda alipokuwa anafundisha timu ya Rayon Sports, kuchukua nafasi ya aliyekuwa kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja aliyeng’atuka.

Alianza kazi chini ya Mcameroon, Joseph Omog lakini akafukuzwa, akaletewa Mfaransa, Pierre Lechantre aliyemalizia msimu na timu ikatwaa ubingwa kabla ya kufukuzwa – na Mbelgiji, Patrick J Aussems anakuwa kocha wa tatu mkuu wa Mrundi huyo. Lakini wakati Lechantre anaondoka alimtupia lawama Juma akidai alimsaliti na inaelezwa alitafuta nafasi ya kuzungumza na Aussems kumueleza juu ya kocha huyo wa Burundi.

Bado uongozi wa Simba SC unasubiriwa kutoa hatima ya Masoud ambaye tangu Oktoba mwaka jana amekuwa Kaimu Kocha Mkuu mara mbili na timu ikaendelea kufanya vizuri.

Masoud alikuwa Msaidizi wa Omog katika mechi 10 tu, timu ikishinda mechi sita, sare tatu na kufungwa moja kwa penalti 4-3 na Green Warriors Mwenge katika hatua za awali za Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.

Baada ya kutolewa na Green Warriors katika Kombe la TFF, Omog akafukuzwa na Masoud akakaimu Ukocha Mkuu, timu ikicheza mechi saba, kushinda nne, sare moja na kufungwa mbili kabla ya ujio wa Kocha mpya Mkuu, Mfaransa Pierre Lechantre.

Na wakati wa Lechantre Simba ilicheza mechi 22 na kushinda 14, sare saba na kufungwa moja kabla ya Mfaransa huyo kuondolewa na Masoud tena kuwa Kaimu Kocha Mkuu akiiongoza timu katika mechi nane na kushinda tano, kufungwa mbili na sare moja. Na wakati huu wa Aussems, pamoja na zile mechi tatu ambazo hakusafiri, SImba imecheza jumla ya mechi 13, ikishinda saba, sare tano na kufungwa moja.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares