Matumaini ya ubingwa Yanga yanavyoingiwa mchanga kitakwimu

201

Jana Jumamosi Aprili 10 vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga walivutwa shati na timu ya Kino Boys KMC kwa kutoa sare ya bao 1-1 mchezo uliopigwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Yanga bado ni vinara wakiwa na alama 51 baada ya sare hiyo. Baada ya sare kocha wa timu Juma Mwambusi aliweka wazi kuwa bado hawajakata tamaa juu ya ubingwa, baadhi ya mashabiki pia wanaamini kuwa ubingwa uko pale pale.
Kimahesabu ni kweli, maana wahenga wanasema “Kheri moja mkononi kuliko mia za kutarajia” Yanga wako kileleni na alama ambazo ZINAWEZA kufikiwa endapo timu zilizopo chini zitachanga karata vyema Azam, Simba, Biashara United n.k.
Faida ambayo Yanga wanayo ni kuwa wanazo alama tayari, klabu zote za chini hazina, lakini zinaweza kufikiwa na Simba kama viporo vyao vinne vitachezwa na itashinda.
Kwa kutumia usemi wa hapo juu, Timu ya Wananchi (Yanga) ina nafasi ya taji la kwanza baada ya ukame wa misimu minne maana mara ya mwisho ilikuwa msimu wa 2014/2015 lakini takwimu zinawakataa?
Mechi saba za mwisho, Yanga imeshinda mara moja tu, sare tano na kipigo kimoja, jumla ya alama 8 pekee zimevunwa badala ya 21, ukitumia takwimu hizi ubingwa kutua Jangwani ni “Bye Bye”.
Spidi ya Kobe itakuwa afadhali kama anayemfukuza ni Kinyonga lakini kama ni Kobe mwezake au nyoka lazima akamatwe tu, Simba wanaoikimbiza Yanga kileleni kwenye mechi saba za mwisho VPL imeshinda tano na kutoa sare mbili. Kwa sasa imecheza mechi 20 inahitaji ushindi wa mechi mbili katika 4 ambazo ni  viporo kuikamata Yanga.
Kama Simba wanahitaji mechi saba kuangusha alama nne na Yanga inahitaji mechi kama hizo kuangusha alama 13, jibu rahisi takwimu zinaipa Simba ubingwa kulinganisha na Yanga, Azam na Biashara United.
Ubora wa timu, Yanga kila siku kwenye raundi ya pili afadhali ya Jana, kiwango kinashuka badala ya kupanda, ukitazama walivyocheza na Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Polisi Tanzania na hata ya KMC utakubaliana nami kuwa kunahitaji maombi na kazi ya ziada kutwaa ubingwa mbele ya ubora wa Simba waliotinga robo fainali wakiwa vinara mbele ya Al Ahly, Vita Club na EL Merreikh.
Ni ngumu kuwa bingwa ila inawezekana ikiwa wachezaji wako angalau watano hawawezi kufunga goli 8 kwa msimu. Hili kwa Yanga mtihani mkubwa kwao, Kocha Jose Mourinho amewai kusema washambuliaji wanakupa alama tatu, mabeki wazuri wanakupa ubingwa, eneo la walinzi Jangwani liko imara, shida ushambuliaji.
Kauli ya mashabiki wa Timu ya Wananchi na Kaimu Kocha mkuu Juma Mwambusi ni kama inawang’ong’a wenyewe juu ya kutokama tamaa.
Na hitimisha kwa kusema, pengine Yanga waje kivingine sana kwenye mechi 10 zilizosalia ili kutwaa VPL 2020/21 hata hivyo hawahitaji ubora wa uwanjani tu bali hata maombi mabaya kwa wanaowakimbiza (Azam + Simba) kwa nyuma.

Author: Asifiwe Mbembela