Mbao FC uso kwa uso na Everton ya England

57

Michuano ya Sportpesa Super Cup ni michuano iliyoanza miaka miwili iliyopita lakini imejizolea umaarufu kwa kasi kubwa katika soka nchini Tanzania kutokana na ubora wa michuano hiyo licha ya kushirikisha timu chache na huchukua muda mfupi kumalizika

Ushindani ni mkubwa katika michuano hii licha ya zawadi nono ya kitita cha Dola za Kimarekani 30,000 ndani ya wiki moja lakini pia timu bingwa inapata bonasi ya kucheza mchezo na timu kutoka England ambayo pia hudhaminiwa na kampuni ya Sportpesa ambayo huendesha michezo ya bahati na sibu.

Gor Mahia ya Kenya ndio timu iliyoonja mafanikio ya michuano hii kwa misimu miwili mfululizo baada ya timu hiyo kuwa bingwa mara zote mbili na kujizolea kitita cha pesa lakini pia imecheza mara moja na timu ya Everton ya England na pia Hull City kutoka England

Mbao FC huenda ikapambana na Everton inayoshiriki ligi kuu ya kandanda ya England unaweza kusema hivyo baada ya Mbao kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Sportpesa Super Cup 2019 inayotaraji kuanza kutimua vumbi Januari 22 jijini Dar-es-Salaam ikishirikisha timu 8 nne kutoka Tanzania na nne kutoka Kenya

Mbao ni timu ndogo ya ligi kuu ya Tanzania lakini imejizolea umaarufu mkubwa katika soka la Tanzania kutokana na timu hiyo kuwabania timu kubwa hasa inapokua katika uwanja wake wa nyumbani CCM Kirumba jijini Mwanza huenda ikaongeza chachu katika michuano hii kwa msimu huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sportpesa, Abas Tarimba amesema kuwa wameamua kuialika Mbao FC kutokana na kuonyesha ushindani kwenye ligi Kuu Tanzania Bara

“Tumeamua kuialika timu ya Mbao kwa kuwa inafanya vizuri kwenye michezo yake ya Ligi Kuu Tanzania, hivyo tunaamini wataonyesha ushindani pia kwenye michuano ya Sportpesa Super Cup msimu huu,”

Mbao FC inakuwa miongoni mwa timu 4 kutoka Tanzania ambazo zitashiriki michuano ya Sportpesa Super Cup timu nyingine ni Simba, Yanga, Singida United za Tanzania na Kenya ni Gor Mahia mabingwa watetezi, Kariobangi Sharks, Bandari FC na AFC Leopards.

Author: Bruce Amani