Mbappe abakia PSG, licha ya fedha nzito ya Real Madrid

Paris St-Germain imeamua kumbakiza mshambuliaji wake raia wa Ufaransa Kylian Mbappe licha ya mchezaji huyo kuonyesha nia yake ya kuondoka klabuni hapo na kujiunga na Real Madrid.

Mbappe, 22, alikuwa anahusishwa kujiunga na Real Madrid kwa dau la pauni milioni 137 sawa na Euro milioni 160 ingawa Mkurugenzi wa Michezo wa PSG Leonardo alisema kiasi hicho cha fedha hakitoshi.

Mbappe amebakia PSG. Mkataba wake unamalizika mwishoni mwa mwezi Juni 2022, kuanzia Januari 2022 atakuwa huru kuzungumza na timu yoyote ile. Si ajabu akaondoka bure mwishoni mwa msimu huu

Wakati Mbappe akibakia klabuni hapo, mtihani mkubwa kwa wamiliki wa klabu hiyo ni kuhakikisha wanampa dili mchezaji huyo lenye nguvu ili kumfanya abakie Parc Des Princes.

Itakumbukwa kocha wa PSG Mauricio Pochettino akizungumza baada ya mchezo wa wikiendi iliyopita alisema “Mbappe ni mchezaji muhimu kwetu na duniani, kuwa naye kwenye timu ni sawa na zawadi”.

Leonardo naye alisema “kama mchezaji ataondoka hatutamzuia lakini lazima aondoke katika njia zetu sahihi”.

Mbappe amefunga goli 135 katika mechi 175 PSG ambapo ameshinda mataji matatu ya Ligi Kuu Ufaransa Ligue 1, matatu Kombe la Ufaransa na kuifikisha klabu hiyo hatua ya fainali Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza.

Kutokana na Covid-19, Real Madrid imeanguka kiuchumi kwa Euro milioni 300 na imeweza kumsajili beki wa Bayern Munich David Alaba kama mchezaji huru, na kiungo wa Rennes Eduardo Camavinga.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares