Mbappe aumia vibaya kifundo cha mguu, hatarini kukosa Ligi ya Mabingwa

309

Mshambuliaji wa Paris St-Germain Kylian Mbappe amepata maumivu ya kifundo cha mguu katika mchezo wa Kombe la Ufaransa dhidi ya Saint-Etienne siku ya Ijumaa huku miamba hiyo ikishinda.

Mbappe, 21, aliondoka uwanjani huku akilia baada ya kufanyiwa faulo mbaya na beki wa Saint-Etienne Loic Perrin ungwe ya kwanza.

Bado haijajulikana kuwa majeruhi hayo yatakuwa ya muda gani, lakini madaktari wa klabu hiyo tajiri Ufaransa wamesema masaa 72 yatatosha kujua ukubwa wa majeruhi na muda wa kukaa nje ya uwanja.

Raia huyo wa Ufaransa katika msimu wa 2019/20 alikuwa tayari amefunga goli 29 katika mechi 33 za mashindano yote.

Licha ya kuwa ulikuwa ni mchezo wa kwanza kuchezwa Ufaransa tangu walipositisha michezo kutokana na janga la virusi vya Corona lakini PSG walionekana kuwa imara na kufanikiwa kushinda dhidi ya Saint-Etienne.

Watacheza dhidi ya Lyon katika fainali ya Kombe la Ufaransa mnamo Julai 31 na kisha Atalanda ya Italia katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mnamo Agosti 12.

Author: Bruce Amani