Mbele ya Rais, Yanga yatoa kichapo kwa Simba

489

Yanga imefanikiwa kuondoka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Simba mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam Leo Jumamosi Julai 3.

Ushindi wa Yanga sio tu kuwanyima ushindi Simba bali kuwapoka alama tatu na kuwanyima nafasi ya kuwa mabingwa wa Ligi Kuu kwani wangeshinda wangetawazwa.

Mchezo wa leo ambapo Simba ilikuwa inahitaji pointi tatu ili kutangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara mambo yalikuwa magumu kwa timu hiyo iliyoshuhudia pointi tatu zikienda Yanga.

Bao la Yanga limefungwa na Zawadi Mauya kwa shuti kali akimalizia mpira wa kujirudia (rebound) nje kidogo ya eneo la hatari ungwe ya kwanza.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha jumla ya pointi 70 ikiwa nafasi ya pili huku Simba ikibakiwa na pointi 73 baada ya kucheza jumla ya mechi 30.

Mchezo huo umeshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan ambaye kwa mara ya kwanza anatazama dabi ya Kariakoo tangia kutangazwa kuwa Rais wa Tanzania.

Author: Asifiwe Mbembela