Mchezaji wa Burundi afariki baada ya kuzirai uwanjani

Mchezaji wa timu ya taifa ya Burundi Faty Papy amefariki dunia nchini Eswatini.

Kiungo huyo wa zamani wa timu ya Bidvest Wits alizirai uwanjani wakati akiichezea timu yake ya Malanti Chiefs dhidi ya Green Mamba.

Mchuano huo wa Ligi Kuu ya Kandanda ya eSwatini PSL ulichezwa katika uwanja wa Killarney mjini Piggs Peak nje ya mji mkuu Mbabane. Kwa mujibu wa rpoti, Papy alizirai uwanjani dakika 15 baada ya mechi kuanza na akakimbizwa hospitali ambako alitangazwa kuwa kafariki duni.

Kijana huyo ana historia ya matatizo ya moyo na wakati mmoja alizirai wakati wa mchuano wa kirafiki wakati akiichezea Wits mjini Johannesburg Desemba 2015. Mabingwa hao wa zamani wa PSL na Papy walisitisha mkataba wao kutokana na wasiwasi kuhusiana na matatizo yake ya moyo mnamo Septemba 2016.

Hata hivyo, alijiunga na Wits akitokea APR ya Rwanda mwaka wa 2012 na akasisitiza kuwa hangestaafu kutoka kandanda.

Papy aliisaidia Burundi kutinga michuano ijayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Misri, na hata alicheza mechi waliyotoka sare ya bao 1 – 1 na Gabon. Alitumaini kuichezea kwa mara ya kwanza Burundi katika tamasha hilo la Afrika.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends