Mchuano kati ya Kenya na Sierra Leone wafutwa

Shirikisho la kandanda Afrika – CAF limeufuta mchuano wa kufuzu katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON kati ya Kenya na Sierra Leone ambao ulitarajiwa kupigwa katika uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi Kasarani jijini Nairobi Novemba 18.

Taarifa ya kitengo cha mashindano cha CAF imesema kuwa sababu ya kufutwa mchezo huo ni kufungiwa kwa Sierra Leone na Shirikisho la Kandanda Duniani – FIFA, ikisema kuwa picha kamili ya Kundi hilo itajulikana punde Kamati Kuu itakapochukua maamuzi kuhusu suala hilo.

Kenya mpaka sasa imeshinda mechi mbili na kutoka sare mechi moja katika Kundi F, kwenye safari yao ya kutaka kutinga fainali za AFCON zitakzoandaliwa nchini Cameroon. Kundi hilo pia linazijumuisha Ghana na Ethiopia. Mara ya mwisho kwa Harambee Stars kushiriki fainali za AFCON ni mwaka wa 2004.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments