Mechi za CAF za Namungo na C.D Primeiro de Agosto kuchezwa Tanzania baada ya sintofahamu kubwa

252

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeamua mechi zote mbili za Kombe la Shirikisho baina ya CD 1 Agosto ya Angola na Namungo FC ya Tanzania zichezwe nchini Tanzania. Uamuzi huo umefanywa baada ya Kamati ya CAF ya Mashindano hayo kubaini kuwa si Agosto wala Namungo iliyohusika moja kwa moja kukwamisha mechi ya kwanza iliyokuwa ichezwe Februari 14 nchini Angola.

Mechi zote mbili zinatakiwa kuchezwa angalau ndani ya saa 72, na ziwe zimechezwa kufikia Februari 26 mwaka huu. Kwa mujibu wa ratiba, CD 1 Agosto itakuwa mwenyeji wa mechi ya kwanza, hivyo itawajibika katika maandalizi yote ikiwemo gharama za maofisa wa mechi hiyo.

Kwa vile makundi ya Kombe la Shirikisho yatapangwa Februari 22, mshindi wa jumla baada ya mechi hizo mbili hatazingatiwa katika viwango (non-ranked) wakati wa upangaji. Mechi hiyo iliahirishwa kwa kile ambacho kilielezwa kuwa Mamlaka ya Angola iliwataka wachezaji wote wawekwe karantini baada ya wachezaji watatu pamoja na kiongozi mmoja wa Namungo kuelezwa kuwa wamekutwa na maambukizi ya Virusi vya Corona (Covid-19).

Author: Asifiwe Mbembela