Mechi zaidi za Bundesliga kuchezwa bila mashabiki

Mechi zaidi za Bundesliga zitachezwa bila mashabiki uwanjani wikiendi hii kwa sababu ya tahadhari ya virusi vya corona. Mechi hizo ni pamoja na Union Berlin dhidi ya vinara wa ligi Bayern Munich Jumamosi, na Eintracht Frankfurt v Borussia Moenchengladbach Jumapili. Mechi kadhaa tayari zimethibitishwa bila mashabiki ukiwemo mtanange wa derby ya Ruhr kati ya Borussia Dortmund v Schalke Jumamosi.

Mchuano wa Europa Legaue wa hatua ya 16 za mwisho kati ya Frankfurt na Basel wakati huo huo utaendelea na mashabiki uwanjani kama ilivyopangwa.

Nchini England, Premier League imesema mchuano wa leo kati ya Manchester City na Arsenal umeahirishwa kama hatua ya tahadhari. Ni mechi ya kwanza katika ligi kuu hiyo ya England kusitishwa kutokana na virusi vya corona.

Ligi zote kuu barani Ulaya sasa zimeathiriwa na mripuko huo. Mechi katika madaraja mawili ya juu ya Ligi Kuu nchini Uhispania zitachezwa bila mashabiki kwa karibu wiki mbili. Ligi kuu ya Ufaransa Ligue 1 ina divisheni ya pili zitakosa mashabiki hadi Aprili 15, wakati ligi nyignine kadhaa za Ulaya zikichukua hatua sawa na hiyo.

Ligi kuu ya Italia Serie A imesitishwa hadi Aprili 3 pamona na michezo mingine yote nchini humo.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends